Rais Ruto aupigia debe ushuru wa nyumba katika ziara yake nchini Tanzania

"Kupitia mpango huu hatutaweza tu kuwapa maskini nyumba bali kuwaapaatia vijana ajira” alieleza Rais William Ruto.

Muhtasari

• Rais Ruto alijivunia ushuru hiyo inayolenga kupunguza idadi ya mitaa ya mabanda nchini nayozidi kukua kila kunapo kucha.

• Rais Ruto aliwaeleza marais hao kuwa mitaa ya mabanda  ni tatizo kuu si tu Kenya bali barani kwa jumla.

Image: FACEBOOK.

Rais William Ruto ameusifia mpango wake wa kuwatoza Wakenya ushuru wa asilimia 1.5 ya mshahara ili kufadhili mpango wa kujenga nyumba za bei nafuu.

Rais Ruto akizungumza wakati wa ziara ya nchini Tanzania katika kongamano la marais barani kuhusiana na Mitaji ya Watu, alijivunia ushuru huo inayolenga kupunguza idadi ya mitaa ya mabanda nchini nayozidi kukua kila kunapo kucha.

“Nchini Kenya tumefanya uamuzi wa kuwatoza wananchi ushuru wa asilimia 1.5 kutoka kwa mishahara yao, hii ni kwa sababu tuko na watu zaidi ya milioni 6 wanaoishi katika mitaa ya mabanda. Kupitia mpango huu hatutaweza tu kuwapa maskini nyumba bali kuwapatia vijana ajira”

Rais Ruto aliwaeleza marais hao kuwa mitaa ya mabanda  ni tatizo kubwa, sio tu nchini Kenya bali barani kwa jumla. Hata hivyo, Rais aliwahimiza marais wengine kuwa tatizo hilo linaweza kubadilishwa kupitia kuwatengenezea watu hao nyumba na kuwaajiri vijana katika ujenzi wa nyumba hizi.

Mnamo tarehe 26 mwaka huu, Rais William Ruto alitia saini muswada wa fedha wa 2023 na kuifanya kuwa sheria baada ya wabunge kuidhinisha hatua za ushuru zinazolenga kufikisha lengo la shilingi trilioni 3. 6.

Muswada huo ulipendekeza Tozo ya Makazi iliyokumbwa na utata huku Wakenya na wanaharakati nchini wakiupinga vikali. Tozo hiyo ambayo awali ilipendekezwa kuwa asilimia 3 pia ilipitishwa baada ya kufanyiwa marekebisho hadi asilimia 1.5 ya malipo ya jumla. Pendekezo hilo aidha liliweza kugeuzwa kuwa kodi.

Pendekezo la awali lilitaka ushuru huo kuwa wa kuchanga na baada ya kipindi cha miaka 7 Wakenya wangeweza kupata hela walizokuwa wakichanga katika mpango huo.

Hata hivyo, Seneta wa Busia Okiya Omtatah aliwasilisha kesi mahakamani alipoiomba mahakama kusitisha kutekelezwa kwa sheria hiyo.

Jaji wa Mahakama ya Juu Mugure Thande, mnamo Ijumaa, Juni 30, alitoa maagizo ya kihafidhina ya kusimamisha utekelezaji wa Sheria ya Fedha ya 2023.

"Nimeridhika kwamba Maombi yanakidhi mtihani wa maagizo ya kihafidhina na ninakubali maombi ya 2 na 3 ya Maombi hadi Julai, 5 wakati kesi imepangwa kutajwa kwa maagizo," ilisoma sehemu ya uamuzi huo.

Jaji Thande aliamuru mlalamishi kuhudumu pande zote akiwemo Waziri wa Hazina Njuguna Ndung'u kabla ya mwisho wa siku, Ijumaa, Juni 30, 2023.