Lori la mafuta lalipuka na kuua dereva Bungoma

Lori hilo lilikuwa likielekea Malaba lilipogonga nguzo ya transfoma ya umeme na kuwaka moto.

Muhtasari

• Afisa mkuu wa polisi wa Bungoma Francis Kooli  huyo wa polisi alitoa wito kwa watumiaji wa barabara hiyo kuwa waangalifu wanapotumia barabara hiyo yenye shughuli nyingi.

Tangi lililolipuka katika ajali ya Bungoma Jumatano asubuhi Picha: TONY WAFULA
Tangi lililolipuka katika ajali ya Bungoma Jumatano asubuhi Picha: TONY WAFULA

Lori la mafuta lililipuka Jumatano asubuhi katika eneo la Sikata kwenye barabara kuu ya Webuye-Malaba na kumuua dereva papo hapo. Kwa mujibu wa shahidi mmoja, ajali hiyo ilitokea mwendo wa saa saa moja unusu asubuhi. 

Shahidi huyo alisema lori hilo lilikuwa likielekea Malaba lilipogonga nguzo ya transfoma ya umeme na kuwaka moto. 

“Tulijaribu kumwokoa dereva ambaye bado alikuwa ndani ya lori lililokuwa likiungua lakini hatukuweza. Inauma sana kwa sababu tulimshuhudia akiungua hadi kufa,” alisema.

Mabaki ya lori lililoteketea. Picha: TONY WAFULA
Mabaki ya lori lililoteketea. Picha: TONY WAFULA

Shahidi huyo zaidi aliwalaumu wazima moto wa kaunti kwa kuchelewa kufika eneo la tukio, akisema kama wangefika mapema dereva angeweza kuokolewa. 

Kulingana na walioshuhudia tukio hilo, lori hilo lilikuwa likijaribu kuipita matatu iliyokuwa ikielekea Kanduyi lakini ikapoteza mwelekeo na kusababisha ajali hiyo. 

Kamanda wa polisi kaunti ya Bungoma Francis Kooli alithibitisha kuwa lori hilo liliacha barabara na kugonga nguzo ya umeme iliyosababisha mlipuko huo lakini akasema kuwa hakuna mtu ndani ya matatu hiyo aliyejeruhiwa. 

 

Kamanda wa polisi wa Kaunti ya Bungoma Francis Kooli katika eneo la tukio Agosti,09,2023. Picha: TONY WAFULA
Kamanda wa polisi wa Kaunti ya Bungoma Francis Kooli katika eneo la tukio Agosti,09,2023. Picha: TONY WAFULA

Hata hivyo, bosi huyo wa polisi alitoa wito kwa watumiaji wa barabara hiyo kuwa waangalifu wanapotumia barabara hiyo yenye shughuli nyingi.Kooli alisema dereva wa lori alifariki dunia baada ya kunaswa ndani ya gari huku juhudi za kumuokoa zikigonga mwamba.

 "Hata kabla ya wazima moto kufika, wakaazi walijaribu kumwokoa lakini hawakuweza kufika kwa sababu ya mlipuko wa moto," Kooli alisema.   

zimamoto walipofika eneo la ajali. Picha: TONY WAFULA
zimamoto walipofika eneo la ajali. Picha: TONY WAFULA

Kumekuwa na ongezeko la ajali za barabarani huko Bungoma, Jumanne, watu watatu walipoteza maisha baada ya trela lililokuwa likienda kwa kasi kuwagonga wanafunzi wawili na kuwaua papo hapo.