logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Mwanadada aliyewazomea viongozi wa Uasin Gishu akataa ofa ya kazi ya seneta Ledama

Mercy alimtaka seneta Ledama kwanza kuwaomba maseneta wenzake kuishinikiza serikali ya Uasin Gishu kurejesha pesa.

image
na Radio Jambo

Makala11 August 2023 - 08:21

Muhtasari


• Ledama alimsifu mhitimu huyo wa Chuo Kikuu cha Kabarak kwa ujasiri wake na kumpa nafasi ya kumfanyia kazi.

•Mercy alimtaka seneta Ledama kwanza kuwaomba maseneta wenzake kuishinikiza serikali ya Uasin Gishu kurejesha pesa.

Olekina alijitoelea kumpa kazi Mercy Tarus

Mercy Tarus, mwanadada ambaye alipata umaarufu baada ya video yake akiwazomea vikali viongozi wa kaunti ya Uasin Gishu kusambaa mitandaoni amekataa ofa ya kazi iliyotolewa na seneta Ledama Olekina.

Siku ya Alhamisi, Ledama alimsifu mhitimu huyo wa Chuo Kikuu cha Kabarak kwa ujasiri wake na kumpa nafasi ya kumfanyia kazi.

“Mercy Tarus ningependa unifanyie kazi, speka moyo wako. Wakati ujao ni wa vijana waaminifu! Wacha tuzungumze,” Ledama aliambia mwanadada huyo kupitia mtandao wa Twitter.

Huku akimjibu seneta huyo wa Narok, Mercy hata hivyo alionekana kukataa kazi hiyo na kutoa masharti ya kutimizwa kabla ya kukubali kufanya mazungumzo na mwanasiasa huyo.

Mhitimu huyo wa chuo kikuu ambaye kwa sasa anafanya kazi ya kuuza uji na mandazi alimtaka seneta Ledama kwanza kuwaomba maseneta wenzake kuishinikiza serikali ya Uasin Gishu kurejesha pesa ambazo walikuwa wamepokea kutoka kwa wazazi kwa ajili ya mpango wa masomo wa ng’ambo uliofeli.

"Bwana. Ledama, kabla hatujaendeleza mazungumzo haya, zungumza na maseneta wenzako ili kuwajibisha Serikali ya Kaunti ya Uasin Gishu na kuwalazimisha KUREJESHA pesa zilizopatikana kwa bidii kwa Raia wa Kenya. Labda baadaye, tunaweza kuzungumza. Vinginevyo, sina la kusema zaidi,” Mercy alijibu siku ya Alhamisi.

Mercy alidokeza kuwa hayuko tayari kufanya kazi na seneta huyo wa ODM kwa sasa lakini akadokeza kuwa katika siku zijazo huenda akakubali ofa ya kazi kutoka kwake.

"Labda basi, tunaweza kufanya kazi kwenye mradi unaofuata kwa sababu kazi yangu itafanyika hapa. Vinginevyo, siwezi kujitolea kwa majukumu mengine," alisema.

Mercy Tarus amekuwa akivuma kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kwa siku mbili zilizopita huku wanamitandao Wakenya wakiendelea kumsifu kwa ujasiri mkubwa  ambao alionyesha wakati alipokuwa akikabiliana hadharani na gavana wa Uasin Gishu Jonathan Bii, seneta Jackson Mandago na naibu gavana John Barorot mnamo siku ya Jumatatu.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved