Mwili wa msusi aliyetoweka Jane Mwende wapatikana umetupwa kwenye shimo la choo Mlolongo

Familia, marafiki na wafanyakazi wenzake wa Mwende wamekuwa kwenye harakati za kumtafuta

Muhtasari
  • Washukiwa hao ambao walikamatwa wiki jana kuhusiana na kutoweka kwa Mwende awali walikuwa wamewahadaa maafisa wa upelelezi katika msitu wa Magongo eneo la Wote kaunti ya Makueni.
  • Cha kustaajabisha ni kwamba yule bibi mwingine hajawahi kuonekana katika mji wa Mlolongo tangu kutoweka kwa Jane.
JANE MWENDE
Image: SCREENGRAB

Msusi aliyetoweka wiki mbili zilizopita amekutwa ameuawa na mwili wake kutupwa kwenye shimo la choo eneo la Mlolongo, kilomita chache kutoka kwenye kituo chake cha kazi.

Kulingana na Citizen Digital Mwili uliokuwa ukioza wa Jane Mwende Mwanzia mwenye umri wa miaka 29 uligunduliwa baada ya washukiwa kuwaongoza polisi kwenye eneo la tukio.

Washukiwa hao ambao walikamatwa wiki jana kuhusiana na kutoweka kwa Mwende awali walikuwa wamewahadaa maafisa wa upelelezi katika msitu wa Magongo eneo la Wote kaunti ya Makueni.

Katika hali ya kushangaza, washukiwa hao baadaye walibadilisha maelezo yaliyowaongoza polisi kuwa ya Kiserian kabla ya kufichua eneo halisi ambapo mwili wa Mwende uligunduliwa huko Mlolongo.

Familia, marafiki na wafanyakazi wenzake wa Mwende wamekuwa kwenye harakati za kumtafuta kijana huyo mwenye umri wa miaka 29 tangu alipotoweka wiki mbili zilizopita—wameenda katika vituo vingi vya polisi, hospitali na hata kwenye vyumba vya kuhifadhia maiti bila mafanikio.

Jane Mwende anasemekana kupokea simu mapema asubuhi ya Ijumaa, Agosti 25 kutoka kwa mtu aliyejifanya mteja aliyehitaji huduma zake za unyoaji nyumbani kwao. Aliondoka asirudi tena.

“Alipigiwa simu asubuhi kitu saa tatu. saa nne..wakati aliondoka alienda hajawai rudi…,” anasimulia Winnie Munyau, mfanyakazi wa saluni.

“Alitoka hapa lakini hakusema anaenda wapi… alichukua tu simu na akaenda…,” aliongeza Jennifer Mwende ambaye pia anafanya kazi katika saluni hiyo.

Wasiwasi ulizidi pale Jane aliposhindwa kuripoti kazini siku iliyofuata. Simu yake ilibaki imezimwa.

Kutoweka kwa Jane kulionekana wazi alipokosa kumchukua mtoto wake kutoka nyumbani kwake Yatta huko Machakos baada ya likizo ya Agosti.

Maafisa wa polisi katika Kituo cha Polisi cha Mlolongo sasa wanachunguza uhusiano unaowezekana kati ya kutoweka kwa Jane na mgogoro wa mapenzi pamoja na kuhusika kwake katika biashara ya mali isiyohamishika.

Inadaiwa kuwa Jane na mwanamke mwingine katika mji wa mlolongo, wamekuwa katika mzozo unaohusisha mwanamume ambaye tayari amehojiwa na polisi.

Cha kustaajabisha ni kwamba yule bibi mwingine hajawahi kuonekana katika mji wa Mlolongo tangu kutoweka kwa Jane.