Polisi wanachunguza kifo cha mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Daystar

Mwili wa mwanafunzi huyo, kwa mujibu wa polisi, uligunduliwa akiwa amekufa kwenye chumba cha kujisaidia.

Muhtasari

•Mwili wa marehemu kulingana na polisi uligunduliwa na wanafunzi wenzake ambao waliingia kwenye chumba cha kujisaidia kwa kuruka kuta za vyoo na kufungua mlango.

• Kisa hicho kiliripotiwa katika kituo cha polisi cha Athi River kama ripoti ya tukio la kujitoa uhai mnamo Septemba 9 saa 3.15 asubuhi.

Image: Maktaba//The Star

Polisi huko Machakos wanachunguza kisa ambapo mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa chuo kikuu cha Daystar alipatikana amuawa katika hali ya kutatanisha huko Athi River.

Mercy Jerono Kwambai, 18, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Daystar, anasemekana alifariki kwa kujitoa uhai chuoni humo mnamo Septemba 8, 2023.

Kisa hicho kiliripotiwa katika kituo cha polisi cha Athi River kama ripoti ya tukio la kujitoa uhai mnamo Septemba 9 saa 3.15 asubuhi. Polisi walisema tukio hilo liliripotiwa na mratibu wa usalama wa Chuo hicho Patrick Darizu.

"Aliripoti kuwa kulikuwa na mwili wa mwanafunzi wa kike wa mwaka wa kwanza ukiwa umelala kwenye dimbwi la damu katika chumba cha kujisaidia katika Chuo Kikuu cha Daystar," ripoti ya polisi ilisema.

"Maafisa wa polisi na DCI walitembelea eneo la tukio na ikabainika kuwa marehemu Mercy Jerono Kwambai alikuwa amejifungia ndani ya choo na kujiua kwa kujichoma kisu upande wa kushoto wa kifua kwa kutumia kisu cha jikoni.

" Mwili wa marehemu kwa mujibu wa polisi uligunduliwa na wanafunzi wenzake ambao walipata kuingia kwa kuruka kuta za vyoo na kufungua mlango.

Tukio hilo lilishughulikiwa na kurekodiwa na maafisa kabla ya mwili kuhamishwa hadi katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Shalom ukisubiri uchunguzi wa maiti.