Waziri Kindiki atoa hakikisho la kukabiliana na Al-shabaab

Hii ni baada maafisa wa polisi kushambuliwa na kuuwawa Lamu

Muhtasari

• "Tumetangaza vita dhidi ya al-Shabaab. Wanaweza kufikiri watatuzidi ujanja lakini tutawaangamiza kama vile tulivyofanya wezi wa mifugo."

• Aidha alikariri kuwa  serikali haitakubali mauaji ya kiholela, akisema "Siku za kutoweka kwa nguvu zimepita zamani."

Waziri wa usalama wa ndani Kithure Kindiki
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI KITHURE KINDIKI Waziri wa usalama wa ndani Kithure Kindiki
Image: KWA HISANI

Waziri wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki amesema kuwa serikali haitalegea katika vita dhidi ya kundi al-Shabaab.

Akizungumza katika Kaunti ya Wajir wakati wa operesheni ya Kaunti Ndogo ya Kotulo huko Tarbaj, Kindiki alitaja kundi la wanamgambo kuwa adui mkubwa wa Kenya.

“Huyo ndiye adui yetu mkubwa kwa sasa. Wamesababisha maafa nchini mwao na wanaleta hiyo Kenya. Tumedhamiria kuwa serikali inayorejesha amani katika eneo la Kaskazini Mashariki,” 

Waziri aliendelea kutema moto kwa ghadhabu akisema;

"Tumetangaza vita dhidi ya al-Shabaab. Wanaweza kufikiri watatuzidi ujanja lakini tutawaangamiza kama vile tulivyofanya wezi wa mifugo."

Waziri Kindiki aliwashauri wananchi wote kufanya kazi na maafisa wa usalama na kupinga majaribio ya makundi ya kigaidi ya kuwafanya vijana kuwa na itikadi kali.

Aliongeza kusema kuwa serikali itawapa maafisa wa usalama vifaa vya kisasa ili kuwalinda dhidi ya wahalifu waliojihami na kuwawezesha kuwalinda Wakenya na mali zao.

Hata hivyo, aliwapongeza maafisa wa usalama kutoka kwa mashirika yote kwa kufanya kazi bila kuchoka na kwa bidii ili kupambana na ukosefu wa usalama katika Mkoa wa Kaskazini Mashariki.

“Baadhi ya maafisa wetu hata wamepoteza maisha na wengine kujeruhiwa na wahalifu waliojihami. Hakuna zawadi ya kutosha kuwaheshimu maafisa wetu kwa bidii yao. Ni wanaume na wanawake wazalendo wanaoipenda nchi yao. Natoa pongezi kwa maafisa hawa wote wanaofanya kazi katika eneo gumu la Kaskazini Mashariki,” 

Aidha alikariri kuwa  serikali haitakubali mauaji ya kiholela, akisema "Siku za kutoweka kwa nguvu zimepita zamani."

Waziri Kindiki alisimamia kuanzishwa kwa makao makuu ya Kaunti Ndogo ya Kotulo na kuteuliwa kwa Naibu Kamishna wa kwanza wa Kaunti Farah Hassan Mohamed.