Mchungaji mmoja kutoka Moi’s Bridge, kaunti ya Uasin Gishu alifikishwa katika mahakama ya Eldoret akishtakiwa kwa kosa la kupatikana na lita 70 za chang’aa.
Kasisi huyo alipatikana akiwa na pombe hiyo haramu Jumatatu na alizuiliwa katika gereza la Eldoret baada ya kukosa kutoa dhamana ya Sh50,000 pesa taslimu.
Isaac Tenge wa kanisa la New Jerusalem Church alifikishwa mbele ya hakimu mkazi mkuu wa Eldoret Rosemary Onkoba na kushtakiwa kwa kosa la kupatikana na pombe ambayo viungo vyake vilikuwa vya kutiliwa shaka.
Hakimu aliamuru aachiliwe kwa dhamana ya pesa taslimu Sh50,000 au bondi mbadala ya Sh100,000 na mdhamini mmoja wa kiasi sawa na hicho. Kasisi huyo hata hivyo alikosa kuafikia pesa hizo.
Tenge alishtakiwa kuwa mnamo Septemba 24, 2023, alipatikana akiwa na pombe haramu, almaarufu chang’aa, nyumbani kwake Moi’s Bridge katika kaunti ndogo ya Soy, kaunti ya Uasin Gishu.
Alikamatwa na timu ya maafisa wa polisi kutoka kituo cha polisi cha Moi’s Bridge kufuatia msako mkali wa kukomesha uuzaji wa pombe haramu katika eneo hilo.
Maafisa wa usalama walivamia nyumba ya mtumishi huyo wa Mungu kufuatia taarifa kutoka kwa wananchi na kuchukua pombe hiyo haramu, tukio ambalo liliwaacha waumini na wakazi wa kanisa lake katika mshangao na kutoamini.
Mchungaji Tenge alionekana kutelekezwa na kundi lake, kwani hakuna waumini wa kanisa hilo waliokuwepo mahakamani isipokuwa mkewe na watoto watatu. Alikana mashitaka yaliyotolewa dhidi yake.
Kasisi huyo aliwekwa ndani ya basi la gereza pamoja na washukiwa wengine na kupelekwa hadi rumande ya Eldoret baada ya kukosa kutoa dhamana.
Awali, pasta huyo alidai mbele ya mahakama kwamba alipata majeraha yaliyotokana na tukio la kukamatwa na maafisa na kuiomba mahakama kwamba alihitaji matibabu ya haraka.
“Mheshimiwa Jaji, maafisa wa polisi walimpiga mke wangu pamoja na mimi na kutusababishia madhara ya mwili. Nahitaji matibabu ya haraka, vivyo hivyo kwa mke wangu,” alidai pasta.
Kesi hiyo imekadiriwa kusikilizwa na kutajwa mnamo Octoba 5 mwaka huu.