Jalang’o atoa maelezo ya ajali iliyomfanya afanyiwe upasuaji

Jalang'o ametoa shukrani kwa waliomtakia afueni ya haraka, kumtembelea na hospitali na waliomtibu.

Muhtasari

•Jumapili asubuhi, Jalang'o alifichua kuwa sasa yuko nyumbani ambapo ataanza safari yake ya wiki sita ya kupona.

•Jalang'o alifichua kuwa alipata ajali alipokuwa akifanya mazoezi na timu ya mpira wa vikapu ya Bunge mnamo Jumanne, Septemba 26.

Mbunge wa Lang’ata Phelix Odiwour almaarufu Jalang’o amezungumza kwa kina kuhusu jeraha lake la mguu baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini.

Mbunge huyo wa muhula wa kwanza alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Nairobi katika siku chache zilizopita na siku ya Jumapili asubuhi alifichua kuwa sasa yuko nyumbani ambapo ataanza safari yake ya wiki sita ya kupona.

"Ninataka kuchukua fursa hii kuwashukuru kila mtu kwa maombi yenu ya Kupona Haraka na ninyi nyote mlionitembelea katika Hospitali ya Nairobi," Jalang’o alisema kupitia mtandao wa Instagram Jumapili asubuhi.

Aliambatanisha taarifa yake na picha yake akiwa amejipumzisha kwenye sofa nyumbani kwake huku mikongojo ya kumsaidia kutembea ikiwa kando. Mguu wake wa kushoto ambao ulijeruhiwa ulikuwa umefungwa ili kumsaidia kupona baada ya kufanyiwa upasuaji.

“Ninataka kushukuru timu nzima ya hospitali ya Nairobi inayoongozwa na Prof. Atinga kwa kazi nzuri na ukarimu wao wa jumla na huduma. Tuko chini lakini hatujatoka! Timu yetu ya Langata yenye uwezo itasimamia masuala ya eneo bunge yakifuatiliwa kwa karibu na mimi mwenyewe. ASANTENI saana!” alisema.

Akizungumzia jeraha lake, alifichua kuwa alipata ajali alipokuwa akifanya mazoezi na timu ya mpira wa vikapu ya Bunge mnamo Jumanne, Septemba 26.

Ajali hiyo ilimsababishia jeraha kubwa kwenye mguu wa kushoto na kupelekea yeye kufanyiwa upasuaji wa kurekebisha sehemu iliyoharibiwa baada ya uchunguzi wa MRI.

"Jumanne iliyopita wakati wa mazoezi yetu ya asubuhi ya mpira wa kikapu ya Bunge nilipata ajali iliyorarua kano zangu, nilifanyiwa upasuaji wa kurekebisha na kurejea nyumbani wakati safari ya wiki 6 ya kupona inaanza," alisema.

Kundi kubwa la watu mashuhuri wakiwemo Mbunge Babu Owino, Akothee, mjasiriamali Alinur Mohamed, mwimbaji Dufla Diligon, DJ Euphorique, Ian Oparanya, Rodgers Kipembe na MCA Abass Khalif walimtembelea mwanasiasa huyo hospitalini wakati alipokuwa amelazwa kwa takriban  siku tatu.