Kenya itapata mafanikio makubwa-Karen Nyamu asema kuhusu operesheni ya Haiti

Nyamu alidokeza kuwa Kenya pia watapata fedha kutokana na kuongoza operesheni ya Haiti.

Muhtasari

•Nyamu amesema kuwa nia ya Kenya kuchukua jukumu la oparesheni hiyo, kwanza itadhihirisha ulimwengu kuwa Kenya ni nchi ya kutegemewa.

•"Kenya ina historia ya kulinda amani na tumehusika katika nchi kama vile Somalia. Huu ni ujumbe wa usalama unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa na nchi nyingine mbali na Kenya zinazohusika," alisema

Karen Nyamu
Karen Nyamu

Seneta wa kuteuliwa Karen Nyamu amesema ana imani kubwa kwamba Kenya itapata mafanikio makubwa kwa kuongoza oparesheni ya usalama  nchini Haiti.

Kama Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Seneti ya Usalama wa Kitaifa, Ulinzi na Uhusiano wa Kigeni, Nyamu amasema kuwa nia ya Kenya kuchukua jukumu la opareseni hiyo, kwanza itadhihirisha ulimwengu kuwa Kenya ni nchi ya kutegemewa.

"Kenya ina historia ya kulinda amani na tumehusika katika nchi kama vile Somalia. Huu ni ujumbe wa usalama unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa na nchi nyingine mbali na Kenya zinazohusika," alisema.

Katika mazungumzo ya moja kwa moja na Runinga ya K24, Nyamu aliongeza kuwa,Nchi ya kenya inasimama kama nchi ya kutegemewa.

"Na kuna nini kwetu? Kenya inajitokeza kama mshirika wa kutegemewa ambayo ni faida kubwa sana kwetu kaama Taifa. Tunatoa kauli kubwa sana kwamba Kenya ni taifa linalotegemewa."

Aliongeza kuwa kando na  kutumwa Haiti, polisi wa Kenya watafaidi na kozi za mafunzo ya hali ya juu zinazowezeshwa na wafadhili wa misheni.

"Kabla ya polisi hawa kwenda Haiti, watapata mafunzo. Tuseme ukweli tunaweza kuwa hatuna vifaa kwa sasa na ndio maana hatuna tarehe ya kupelekwa lakini mafunzo yatakuwa mazuri kwa vikosi vyetu," Seneta alisema.

Aidha, Nyamu alidokeza kuwa Kenya pia itapata fedha kutokana na kuongoza operesheni ya Haiti.

"Motisha za kifedha pia zinahusika. Tunapozungumza hivi sasa Marekani na nchi nyingine zinazotaka kusaidia misheni zimetoa dola milioni 200 kwa misheni hii," alisema.

Aliongeza kwa kueleza majukumu ya kikosi kitakachotuma kwenye operesheni hiyo akisema Kikosi cha Kenya,kinakusudiwa kuimarisha sheria na utulivu wa sehemu hizo.

"Kwa hiyo kuna mengi tunapaswa kupata. Kenya haitaingia vitani, maafisa wetu hawatakuwa wamebeba bunduki ili kukabiliana na magenge. Wanaenda kwenye vituo vya watu kama viwanja vya ndege, hospitali na benki; wanakwenda kuimarisha sheria na utulivu. Hawaendi kwenye mashambulizi."