KNEC yatoa orodha ya vifaa visivyo hitajika katika kumbi za mitihani

Mtihani wa KCPE wa 2023 utaashiria mwisho wa mfumo wa 8-4-4 katika shule za msingi

Muhtasari

•Mitihani ya KCSE itaanza Oktoba 23 na kukamilika Novemba 24,Mazoezi yatafanyika Oktoba 19, Tarehe ya mazoezi ya KCPE na KPSEA imepangwa kuwa Ijumaa, Oktoba 27

Wanafunzi wa darasa ya 5 wakifanya mtihani wa kitaifa uliopita mnamo 2022 Picha: FILE
Wanafunzi wa darasa ya 5 wakifanya mtihani wa kitaifa uliopita mnamo 2022 Picha: FILE

Baraza la Kitaifa la Mitihani la Kenya (KNEC)  limetoa orodha ya vifaa ambavyo havifai kupatikana katika kumbi za mtihani.

Katika chapisho kwenye  mtandao wa X (Twitter) Jumatano  baraza linasema  kuwa hakuna kifaa cha kielektroniki kinachofaa kupatikana katika ukumbi wa mtihani.

Miongoni mwa vifaa vya kielektroniki vilivyopigwa marufuku katika chumba cha mtihani ni simu za mkononi, saa za kisasa, kalamu za kamera,  chochote kinachoweza kuunganishwa na kingine kupitia spika za masikioni, mikoba,  knec ilisema.

 

Wanafunzi wanatakiwa  pia kujiepusha kuwa na maandishi kwenye nguo au viatu vyao.

Saa za mkono pia haziruhusiwi katika chumba cha mtihani,Kwa wanafunzi walio na tattoo kwenye miili yao, Knec inawataka wajiadikishe  kwa kuwa hakuna mwanafunzi anayeruhusiwa kuwa na maandishi kwenye miili yao wanapoingia kwenye chumba cha mtihani.

 Miongozo hiyo ilitolewa wakati ambapo watahiniwa kote nchini wanajiandaa kufanya mitihani yao ya kitaifa  KCPE na KCSE.

Zaidi ya watahiniwa milioni 3.5 watafanya mitihani ya kitaifa huku watahiniwa wa KCPE wakichukua idadi kubwa zaidi kuwahi kurekodiwa nchini.

Watahiniwa karibu milioni moja tu ndio watafanya mitihani ya KCSE mwaka huu huku milioni 1.4 watafanya mitihani ya KCPE.

Mitihani ya KCSE itaanza Oktoba 23 na kukamilika Novemba 24,Mazoezi yatafanyika Oktoba 19, tarehe ya mazoezi ya KCPE na KPSEA imepangwa kuwa Ijumaa, Oktoba 27.

Mitihani ya KCPE na KPSEA itaanza Jumatatu, Oktoba 30, na kumalizika Jumatano, Novemba 1.

Mtihani wa KCPE wa 2023 utaashiria mwisho wa mfumo wa 8-4-4 katika shule za msingi.

 

Kwa sasa, Knec inajitahidi kuhakikisha kuwa hakutakuwa na visa vya utovu wa nidhamu katika mitihani ya kitaifa ya 2023.