Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangula amefichua mpango wa serekali kujenga bandari kavu Bungoma, akisema wamekubaliana na Rais William Ruto .
Wentangula amesema kuwa mradi huo utatekelezwa ili kusaidia kurahisisha uondoaji wa mizigo na usafirishaji wa bidhaa kati ya nchi jirani.
"Tuna kipande cha ardhi cha ekari 150 hapa kinachomilikiwa na Mamlaka ya Bandari ya Kenya na tutaweka bandari kavu," alisema.
Akizungumza Teso Kaskazini siku ya Jumamosi, Wetangula aliahidi zaidi kusaidia ujenzi wa njia ya reli ya Standard Gauge (SGR) kutoka Bungoma hadi Malaba.
Kwa mujibu wa Spika, njia ya reli itajengwa kama ilivyopangwa awali,kwa lengo la kuimarisha maendeleo ya kiuchumi katika eneo hilo pamoja na kutengeneza ajira kwa vijana.
"Utawala uliopita ulibadilisha njia isiweze kupita hapa lakini tumeigeuza na kwa hivyo ujenzi sasa utaendelea kutoka Naivasha ambapo ," alisema.
Awamu ya 1 ya mradi huo ambayo ni kilomita 485 ilianza kutoka Mombasa na kuishia Nairobi ukigharimu Sh327 bilioni huku awamu ya 2A ambayo ni kilomita 120 ikitoka Nairobi hadi Naivasha ikigharimu Sh150 bilioni.
Serikali inapanga kutumia Sh2.1 trilioni kurefusha njia ya reli kutoka Suswa hadi Malaba na njia ya reli tofauti hadi Isiolo, miradi inayotarajiwa kukamilika 2027.
Kandarasi za kibiashara za sehemu ya SGR ya Naivasha-Kisumu na Kisumu-Malaba nchini Kenya zimetiwa saini ,huku mkataba wa kibiashara wa sehemu ya SGR ya Malaba-Kampala nchini Uganda utatiwa saini hivi karibuni , serikali hizo mbili ziko katika harakati za kuhamasisha ufadhili wa ujenzi, ” taarifa ya pamoja ya mawaziri husika ilisomeka.