Ziara ya kamati ya seneti kwa Kanisa la mhubiri Ezekiel yaibua maswasli

Kuna madai kwamba huenda ziara ya maseneta hao ilifadhiliwa na kanisa la Mchungaji Odero.

Muhtasari

• Seneta wa Tana River na mwenyekiti wa kamati hiyo Danson Mungatana aliitetea kamati hiyo akisema walichofanya ni kujaribu kutafuta ukweli.

katika kanisa la Mchungaji Ezekiel Odero huko Mavueni, kaunti ya Kilifi, Jumatatu, Oktoba 16, 2023.
Kamati maalum ya Seneti kuhusu mauaji ya Shakahola katika kanisa la Mchungaji Ezekiel Odero huko Mavueni, kaunti ya Kilifi, Jumatatu, Oktoba 16, 2023.
Image: JOHN CHESOLI

Maswali yameibuka kuhusiana na ziara ya baadhi ya wanachama wa kamati maalumu seneti ambayo inachunguza mkasa wa shakahola kuhusiana na ziara yao katika kanisa la New Life lake mhubiri Ezekiel Odero.

Baadhi ya maseneta wameshtumu wenzao kwa kutembelea Kanisa la New Life la Mchungaji Ezekiel Odero katika kaunti ya Kilifi.

Kamati hiyo inayoongozwa na Danson Mungatana, ilizuru kanisa la Mchungaji Odero wikendi ili kubaini baadhi ya madai yaliokuwa yamelimbikiziwa kanisa hilo.

Kuna madai kwamba huenda ziara ya maseneta hao ilifadhiliwa na kanisa la Mchungaji Odero.

Inasemekana Maseneta hao walisafiri hadi Mombasa bila maafisa wa bunge na hivyo kwenda kinyume na kanuni za bunge.

Seneta wa Tana River na mwenyekiti wa kamati hiyo Danson Mungatana aliitetea kamati hiyo akisema walichofanya ni kujaribu kutafuta ukweli.

“Tuliambiwa kuna makaburi kwenye eneo la tukio, tukaenda kukagua, hakuna, tukaambiwa kuna chumba cha kuhifadhia maiti, tukakagua hakuna, ndiyo tu tulikwenda kufanya”, Mungatana alisema.

Kamati hiyo ambayo imeratibiwa kuwasilisha ripoti yake siku ya Alhamisi ilikosa kuandaa kikao cha Jumanne baada ya mshukiwa mkuu Paul Mackenzie au mwakilishi wake kukosa kufika.

Mkasa wa Shakahola umeacha wengi vinywa wazi baada ya zaidi ya miili 400 ikiwemo ya watoto kufukuliwa katika makaburi ya kisiri ndani ya msitu wa Shakahola. Kiongozi wa kanisa la Good News International Paul Mackenzie na baadhi ya wafuasi wake wamekuwa korokoroni wakikabiliwa na mashtaka kadhaa ya mauaji miongoni mwa mshtaka mengine mengi.