logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Tatizo letu humu nchini ni gharama ya mafuta-Mbunge Salasya asema

Tukiweza kupunguza bei ya mafuta, nakwambia bure hutataka kuondoka Kenya

image
na Davis Ojiambo

Habari24 October 2023 - 12:45

Muhtasari


  • •Salasya alitoa wito kwa wananchi kuipenda nchi yetu kwani aliitaja kuwa bora na yenye mazingira mazuri kwa watu.
  • •Mbunge huyo amekuwa katika ziara katika mataifa kadhaa ya Afrika na hakusita kubainisha kuwa kila mahali alipotembelea, gharama ya maisha inamkumbusha kuwa Kenya ndiyo nchi bora zaidi kuishi.
Mbunge wa Mumias mashariki Peter Salasya

Mbunge wa Mumias Mashariki Peter Salasya amedai kuwa Kenya ndiyo nchi bora zaidi kuishi ikilinganishwa na mataifa mengine ambayo amewahi tembelea hasa kwa suala la gharama ya maisha.

Kwenye akaunti yake ya X alieleza kuwa alilinganisha bei ya viatu alivyokuwa amevaa akisema vinagharimu Shilingi 4000 zaidi nchini Afrika Kusini ikilinganishwa na Kenya.

"Ndio Taifa la Afrika Kusini limeendelea lakini maisha ni ghali, viatu hivi ninavivaa vinagharimu Shilingi 5,000 wakati hapa Cape Town ni Randi 900 ambazo ni sawa na shilingi 9,000 za Kenya," Salasya alisema.

Mbunge huyo amekuwa katika ziara katika mataifa kadhaa ya Afrika na hakusita kubainisha kuwa kila mahali alipotembelea, gharama ya maisha inamkumbusha kuwa Kenya ndiyo nchi bora zaidi kuishi.

Aliongeza kuwa ikiwa gharama ya mafuta itapunguzwa nchini Kenya, hakuna mtu ambaye angetaka kuondoka kwenda mataifa mengine.

"Tatizo letu Kenya ni mafuta tu, tukiweza kupunguza bei ya mafuta, nakwambia bure hutataka kuondoka Kenya. Nilikuwa Ghana, Morocco, Tanzania, Sudan Kusini sasa Afrika Kusini," Salasya alisema. .

Salasya alitoa wito kwa wananchi kuipenda nchi yao kwani aliitaja kuwa bora na yenye mazingira mazuri kwa watu.

Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Petroli nchini (EPRA) ilitangaza katikati mwa Oktoba  ongezeko la bei ya mafuta hadi kiwango cha juu katika historia ya nchi, na lita moja ya petroli sasa inauzwa kwa Shilingi 218.

Kupanda kwa bei ya mafuta kwa upande wake kulisababisha kupanda kwa bei za bidhaa zingine, hatua iliyoibua mijadala mbalimbali kutoka kwa wananchi waliolalamikia gharama ya juu ya maisha.

Kenya na Afrika Kusini zimekuwa zikikabiliwa na ongezeko la gharama ambalo limechangiwa na mzozo wa ongezeko la mafuta duniani.

Kulingana na utafiti, inakadiriwa kuwa Afrika Kusini ni karibu asilimia 14 ya gharama zaidi kuliko Kenya.

Ripoti za eNCA, Televisheni ya Afrika Kusini mnamo Septemba 12, 2023, zilionyesha baadhi ya wananchi wakilalamika huku bei ya mafuta nchini humo ikipanda.

Bei ya mafuta nchini iliongezeka kwa kiasi na kusababisha ongezeko la bei za bidhaa za msingi kama vile chakula, usafiri na gharama za umeme kuwaacha wengi kwenye njia panda.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved