Matukio yaliyoripotiwa siku ya kwanza ya mitihani ya KCPE na KPSEA

Haya yanajiri huku ripoti zikionyesha kuwa wafungwa 13 kutoka gereza la Naivasha walikosa kufanya mitihani siku ya Jumatatu.

Muhtasari

•Katika visa vingine vilivyoripotiwa katika siku ya kwanza ya mitihani ya KCPE na KPSEA, wanafunzi watatu wa kike wanaripotiwa kuandika mitihani yao hospitalini baada ya kujifungua.

•Katika kisa kingine, mtahiniwa mwenye umri wa miaka 17 kutoka shule moja huko Kitui Magharibi alilazimika kuandika mitihani yake kutoka hospitalini baada ya kujifungua siku ya Jumapili.

Maafisa wa Kitui wamezidisha msako wa kumtafuta msichana wa miaka 17 ambaye alitoweka nyumbani kwao Jumatatu asubuhi.

Kulingana na ripoti ya polisi, msichana huyo alistahili kufanya mitihani yake ya KCPE katika shule ya msingi huko Kitui.

Alitoweka nyumbani kwao pamoja na mtoto wake wa miezi mitatu na hivyo kukosa mitihani yake.

Tukio hilo limeripotiwa katika kituo cha polisi cha Kabati na juhudi za kumtafuta aliko zimeanza.

Katika visa vingine vilivyoripotiwa katika siku ya kwanza ya mitihani ya KCPEna KPSEA, wanafunzi watatu wa kike wanaripotiwa kuandika mitihani yao hospitalini baada ya kujifungua.

“Mtahiniwa mmoja wa KCPE alijifungua leo katika hospitali ya mama na mtoto Wote iliyoko Makueni. Kwa sasa anafanyia mitihani yake katika kituo hicho chini ya ulinzi,” ripoti ya kisa hicho ilisema.

Katika kisa kingine, mtahiniwa mwenye umri wa miaka 17 kutoka shule moja huko Kitui Magharibi alilazimika kuandika mitihani yake kutoka hospitalini baada ya kujifungua siku ya Jumapili.

"Amesaidiwa vyema na sasa anafanya karatasi yake ya hisabati hospitalini," ripoti hiyo inasoma.

Katika kisa sawia kilichoripotiwa Mwingi, mtahiniwa mmoja katika mojawapo ya shule alipata uchungu wa kuzaa na kukimbizwa hospitalini ambako alijifungua salama.

"Mipangilio imefanywa na anafanya anafanyia mitihani yake katika kituo hicho," ripoti hiyo inasema.

Hata hivyo, katika hali tofauti, mwanafunzi wa kiume wa darasa la sita kutoka Shule ya Msingi ya Ngumbwa huko Mutitu alilazimika kufanya mtihani wake wa KPSEA katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Kitui baada ya kulazwa kutokana na kuvunjika miguu.

Haya yanajiri huku ripoti zikionyesha kuwa wafungwa 13 kutoka gereza la Naivasha walikosa  kufanya mitihani siku ya Jumatatu.

Wafungwa hao hawakuachiliwa au kuhamishiwa katika taasisi nyingine za adhabu wakati gereza hilo likiwa limesajili jumla ya watahiniwa 54 wa mitihani ya kitaifa.

Kati ya idadi hiyo, ishirini na moja wanatumikia kifungo cha maisha jela katika gereza hilo ambalo lina zaidi ya wafungwa 3,000 ambao wengi wao wako chini ya mpango wa elimu.

Kulingana na afisa anayesimamia gereza hilo Hassan Tari wafungwa hao wote walikuwa tayari kwa mitihani licha ya changamoto mbalimbali.

Takriban watahiniwa milioni 1.4 wanafanya mitihani ya mwisho ya KCPE chini ya mtaala wa 8-4-4 ambao umekuwepo tangu 1985.