Uchunguzi wa kina umeanza baada ya maafisa wa polisi mjini Ongata Rongai kupata magunia 26 ya bangi yaliyofichwa ndani ya kanisa moja eneo la Kware. Thamani ya mihadarati hiyo inakadiriwa kuwa Sh6,240,000.
Maafisa hao wa usalama pia walipata mzoga wa mbuzi ambaye alikuwa ameripotiwa kutoweka na kuchinjwa ndani ya kanisa hilo.
Kamanda wa polisi wa Kaunti ndogo ya Kajiado Kaskazini, Abduba Hussein, alisema polisi walichukua hatua kutokana na taarifa kutoka kwa wananchi.
Alisema washukiwa hao waliokamatwa ni waumini wa kanisa la mtaani linalojulikana kama African B Divine Church.
"Wawili hao walikuwa wamechinja mbuzi wa Jessie Muthiga Albert na walipatikana wakiwa wamehifadhiwa katika kanisa hilo," kamanda wa polisi alisema.
Hussein alisema chifu wa eneo hilo, Esther Njeri, alipata habari kuwa washukiwa walikuwa wakiendesha biashara haramu katika kanisa hilo.
Bosi huyo wa polisi alisema washukiwa hao wawili waliokolewa kutoka kwa wananchi waliokuwa na hasira baada ya kupigwa kitutu vibaya.
"Wawili hao walikimbizwa katika hospitali ya Saitoti iliyoko Ongata Rongai, ambapo walilazwa wakiwa katika hali mbaya," Hussein alisema.
Alisema kesi hiyo imechukuliwa na maafisa wa DCI kutoka Ongata Rongai kwa uchunguzi na washukiwa wanatarajiwa kufikishwa mahakamani.