Seneta wa Narok Ledama Olekina sasa anasema kuwa Waingereza waliiacha Kenya nchi bora kuliko walivyoipata.
Akizungumza na runinga ya Citizen, Ledama alisisitiza kuwa huu si wakati wa watu kuwasilisha madai kwa Mfalme wakati kuna matatizo makubwa yanayohitaji kutatuliwa.
Seneta huyo alisema wakati mabwana wa kikoloni walipofanya ukatili dhidi ya Wakenya, Mfalme Charles III alikuwa kijana.
Ledama alisema ni wakati umefika Wakenya kupata uhalisia na kufahamu kwamba walipaswa kudai zaidi kutoka kwa mamake Mfalme marehemu Malkia Elizabeth.
"Ukweli usemwe, Waingereza waliiacha nchi hii mahali pazuri kuliko walivyoikuta, walipokuja tulikuwa taifa kati ya mataifa. Kuanzia sasa tuwe wakweli na tuseme alipokua na mama malkia, labda tungemdai mengi," Seneta alisema.
" Sidhani ni wakati wa sisi kudai mambo fulani yafanyike. Alikuwa mdogo sana wakati tunapata uhuru wetu, najua kwa sisi Wamasai tunaweza kudai wafungue tena kitabu cha Lancaster na tusaini ili tujisikie kuwa tuko huru kabisa, lakini ni kitu gani ambacho kinaweza kutusaidia leo?"
Seneta huyo wa Narok alibainisha kuwa anafahamu kuwa kuna Wamasai nchini Kenya na Tanzania wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo kufukuzwa katika mashamba yao, lakini huu ni wakati wa kufikiria nini kifanyike kuwasaidia watu hao.
Ledama aliwataka mawakili waliokuwa mahakamani wakiwakilisha makundi mbalimbali yaliyokuwa yakitoa madai kwa Mfalme na kuyataja kuwa ni ya ubinafsi na kwamba walikuwa wakitafuta pesa tu.
Aliongeza kuwa hata watu waliolipwa fidia na Waingereza kutokana na ukatili wa huko nyuma, hela walizopata ziliingia kwenye mifuko ya mawakili na ni kidogo sana ikilinganishwa na maumivu waliyopitia.
“Kama tunapigania kulipwa fidia niambieni hii ni fidia gani, hizo vita za mahakamani ni porojo tu za mawakili kutafuta pesa, jiulize hao elfu tano waliolipwa fidia, fedha nyingi zilikwenda kwa mawakili.
"Ukweli ni kwamba, ni kitu gani tunaweza kufanya kwa sasa? Je, tunaweza kujaribu kufanya mazungumzo kwa ajili ya mipango bora ya elimu kwa watu wetu? Je, tunaweza kuingiza maslahi yake? Jambo moja ambalo ni lazima tuliweke wazi katika nchi hii ni kwamba sisi si ombaomba. "