Mfalme Charles III, Camilla waondoka Kenya kurudi Uingereza kupitia Mombasa

Mfalme Charles na Malkia Camilla wameondoka Kenya kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Moi.

Muhtasari

•Mfalme na mkewe walionekana na Rais William Ruto na Naibu wake Rigathi Gachagua katika uwanja wa ndege wa Mombasa.

•Mke wa Rais, Rachel Ruto na Malkia Camilla walitembea kwa ukaribu nyuma huku pia wakishiriki mazungumzo madogo.

akizindikizwa na rais Ruto katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Moi.
Mfalme Charles akizindikizwa na rais Ruto katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Moi.
Image: TWITTER// NESH MAINA

Baada ya kukaa siku nne nchini Kenya, Mfalme Charles na Malkia Camilla wameondoka Kenya kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Moi.

Mfalme huyo wa Uingereza na mkewe walionekana na Rais William Ruto na Naibu wake Rigathi Gachagua katika uwanja wa ndege wa Mombasa.

Mvua nyepesi ilishuhudiwa huku Ruto akitembea pamoja na Mfalme kwenye zulia jekundu walipokaribia njia ya kupandia ndege.

Wote wawili walikuwa wakijikinga na mvua kwa miavuli.

Mke wa Rais, Rachel Ruto na Malkia Camilla walitembea kwa ukaribu nyuma huku pia wakishiriki mazungumzo madogo.

Mapema siku hiyo, Mfalme Charles III alizuru kanisa kuu la Mombasa Memorial huku kukiwa na ulinzi mkali kutoka kwa serikali ya Kenya na Uingereza.

Pia alikutana na Viongozi wa Imani katika Chapeli ya Wanawake kabla ya kuketi pamoja na wanachama wengine kumi wa Baraza la Viongozi wa Dini Mbalimbali la Pwani.

Wanandoa hao wa kifalme walifika Mombasa siku ya Alhamisi ambapo Mfalme alipokelewa na Rais Ruto katika kituo cha majini cha Mtongwe na kukagua walinzi wa heshima.

Mfalme Charles III alikagua ulinzi uliokuwa umepandishwa na Jeshi la Wanamaji la Kenya kabla ya kushuhudia Makomandoo wa Wanamaji wa Kenya (KNMC) wakifanya mazoezi ya kutua kwenye jeti ya Mtongwe.

Baadaye, alikuwa Nyali ambapo Mfalme alizawadiwa kiti na vijana wa Mombasa.

Kiti cha Kiswahili cha plastiki kilitengenezwa kwa chupa za plastiki zilizorejeshwa ambazo hutupwa na watu wanaotembelea fukwe.

Mfalme Charles III alituzwa kama shujaa wa Tide Turner nchini Kenya na kukabidhiwa beji pia.