Bei ya petroli huenda ikapanda hadi Sh300- Waziri Chirchir

Kwa sasa bei ya petroli inauzwa kwa Sh217 jijini Nairobi

Muhtasari

•Kupanda kwa bei ya mafuta kwa upande wake kutasababisha kupanda kwa bei za bidhaa nyingine, hatua iliyoibua kejeli mbalimbali kutoka kwa wananchi waliolalamikia ughali wa maisha.

Mhudumu akiweka gari Mafuta
Mhudumu akiweka gari Mafuta
Image: MAKTABA

Waziri wa Nishati Davis Chirchir amesema kuwa  huenda bei ya mafuta ya super petroli ikaongezeka hadi  kufikia shillingi  mia tatu ikiwa bei ya kimataifa itaongezeka.

"Bei za kimataifa za mafuta zinaweza kupanda hadi dola 150,Hii inamaanisha kuwa bei zetu za petroli zinaweza kupanda hadi Sh300 kwa lita kwenye Bomba,Tunatumai haitafika huko," alisema.

Waziri huyo alisema hayo  alipokuwa  akizungumza  mbele ya kamati ya Mazungumzo ya Kitaifa  Bomas of Kenya Jumatatu.

Katikati mwa mwezi Oktoba, Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Petroli nchini Kenya ilitangaza  bei mpya ya mafuta hadi rekodi ya juu katika historia ya nchi, lita moja ya petroli sasa ikiuzwa kwa Sh217.

Kupanda kwa bei ya mafuta kwa upande wake kutasababisha kupanda kwa bei za bidhaa zingine, hatua iliyoibua kejeli mbalimbali kutoka kwa wananchi waliolalamikia ughali wa maisha.

Kenya na Afrika Kusini zimekuwa zikikabiliwa na ongezeko la gharama ambalo limechangiwa na tatizo la ongezeko la mafuta duniani.

Kulingana na Mtazamo wa hivi karibuni wa Masoko ya Bidhaa  mzozo wa Israel na Gaza umechangia pakubwa  katika bei ya bidhaa  kupanda kutokana na kukatika kwa mzunguko wa kimataifa wa usambazaji bidhaa.