Tutafanya haki kuhusu swala zima la kubanduliwa kwa Mwangaza - Sifuna

Gavana huyo alitimuliwa Jumatano iliyopita baada ya MCA 59 kupiga kura kuunga mkono hoja ya kumtimuliwa.

Muhtasari

• Katika taarifa yake siku ya Jumatatu, Sifuna alisema amepokea maelezo ya kesi hiyo na uamuzi utaafikiwa kulingana na sheria na ushahidi uliowasilishwa.

• "Nimepokea karatasi za mashtaka katika kesi ya Meru,ile ya bunge la Kaunti pamoja na majibu ya Gavana,"

Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna
Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna

Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna amewahakikishia wakaazi wa Meru kuwa Bunge la Seneti litafanya kile ambacho ni sawa, katika swala la  kumtimua Gavana Kawira Mwangaza.

Katika taarifa yake siku ya Jumatatu, Sifuna alisema amepokea maelezo ya kesi hiyo na uamuzi utaafikiwa kulingana na sheria na ushahidi uliowasilishwa.

"Nimepokea karatasi za mashtaka katika kesi ya Meru,ile ya bunge la Kaunti pamoja na majibu ya Gavana,"alisema.

"Ninataka kuwahakikishia wakazi wa Meru kwamba Seneti inachukulia jukumu lake katika mchakato huu kwa uzito mkubwa na mnaweza kuamini kwamba tutafanya yaliyo sawa kulingana na sheria na ushahidi ulio mbele yetu," aliongeza.

Matamshi yake yanakuja huku Mwangaza anayekabiliwa na mzozo akisubiri kujitetea mbele ya Seneti kwa mara ya pili katika muda usiozidi mwaka mmoja.

Maseneta mnamo Alhamisi waliidhinisha hoja ya kitaratibu ya kubadilisha saa za vikao vya Novemba 7 na 8 ili kuendesha vikao vya mapendekezo ya kuondolewa afisini kwa kung'atuka kwa gavana.

Hoja ya kiongozi wa wengi Aaron Cheruiyot iliungwa mkono na seneta wa Kilifi Steward Mwadzayo na kuidhinishwa kwa kauli moja na wanachama.

Maseneta sasa watakutana kuanzia 9:00 asubuhi hadi 1.00 jioni kwa vikao vya asubuhi na saa 2:30 alasiri hadi mwisho wa shughuli za vikao vya alasiri katika siku hizo mbili.

Uamuzi wa kusikilizwa kwa kikao hicho ulifikiwa Jumanne baada ya wanachama kukataa ombi la Seneta wa Narok Ledama Ole Kina.

Ole Kina aliunga kamati hiyo mkono katika kuchunguza madai ya kumtimua gavana Mwangaza.

Gavana huyo alitimuliwa Jumatano iliyopita baada ya MCA 59 kupiga kura kuunga mkono hoja ya kumtimuliwa.

Mwangaza anakabiliwa na madai kadhaa ambayo yakidhibitishwa na  Senetiyatapelekea kubanduliwa madarakani.

Katika shtaka la kwanza, gavana huyo anatuhumiwa kwa ubadhirifu na matumizi mabaya ya rasilimali za umma.

Pia anadaiwa kulipa mishahara na marupurupu kwa maafisa wa ngazi za juu bila kutoa huduma zozote kwa kaunti.

Gavana huyo alikabiliwa na shtaka lingine la upendeleo wa kindugu na utovu wa maadili huku Bunge likidai aliwakilisha jamaa wasio na sifa kama wafanyikazi wa kiufundi waliohitimu kwa ukaguzi wa vifaa vya matibabu nchini China.

Shtaka la tatu ni dhuluma, kuwatukana na kuwadhalilisha viongozi wengine wa kaunti na matatizo yake huku naibu wake akiwasilishwa kama ushahidi.

Katika shtaka la nne, gavana huyo anatuhumiwa kwa uteuzi usio halali na unyakuzi wa mamlaka ya kisheria.

Pia anadaiwa kudharau mahakama, akiitaja barabara ya umma kinyume cha sheria kwa jina la mumewe na kudharau Bunge la Kaunti.