Mpuru Aburi akana matamshi kwenye video iliyochezwa seneti, amtaka gavana Mwangaza aombe msamaha

Mbunge Mpuru Aburi amejitokeza kujitetea akisema video ambayo ulichezwa wakati wa kesi ya gavana Mwangaza ilihaririwa.

Muhtasari

•Mbunge Mpuru Aburi amedai kuwa video iliyotumiwa katika Bunge la Seneti wakati wa kesi ya kubanduliwa madarakani kwa Gavana Kawira Mwangaza ilihaririwa ili kukidhi maslahi yake.

•Mbunge huyo alisema kuwa yeye kama mzazi hawezi kutamka maneno hayo kwa kuwa ana mabinti na wakwe.

Mbunge Mpuru Aburi
Image: MAKTABA

Mbunge wa Tigania Mashariki, Mpuru Aburi amedai kuwa video iliyotumiwa katika Bunge la Seneti wakati wa kesi ya kubanduliwa madarakani kwa Gavana wa Meru Kawira Mwangaza ilihaririwa ili kukidhi maslahi yake.

Akizungumza kwa mara ya kwanza baada ya kukashifiwa na baadhi ya Wakenya kuhusu video hiyo, mbunge huyo alikanusha matamshi ambayo yalisikika kwenye video hiyo.

Katika video iliyochezwa katika Bunge la Seneti, Mbunge Aburi alisikika akitamka maneno yasiyoweza kuchapishwa katika lugha ya Kimeru, akionekana kumlenga Gavana Mwangaza.

Matamshi hayo yalisambaa kwenye mitandao ya kijamii yakivuta hisia miongoni mwa Wakenya na mashirika ya kiraia ambao walitaka kuchukuliwa hatua za kisheria dhidi ya mbunge huyo.

Hata hivyo, siku ya Ijumaa mbunge huyo alijitokeza kujitetea akisema video hiyo ilihaririwa.

Mbunge Aburi sasa anasema ataandikisha taarifa katika Kurugenzi ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kwa madai ya kukashifu.

"Mimi Mpuru Aburi nina imani na kina mama, na ninaenda kwa DCI kuandika statement kuhusu defamation ambayo imefanyika kwa Seneti yetu ya Kenya. Ile video ilionyeshwa katika bunge ilikuwa edited. Ile maneno yote niliongea niko nayo kwa simu yangu," alisema.

Mbunge huyo alisema kuwa yeye kama mzazi hawezi kutamka maneno hayo kwa kuwa ana mabinti na wakwe.

Alitaka ombi la msamaha kutoka kwa Gavana Mwangaza akidai kuwa alihariri video hiyo ili kukidhi maslahi yake.

Matamshi hayo yanayodaiwa kuwa ya mbunge Aburi yalivutia shutuma nyingi katika seneti huku wachanganuzi wakisema ni sehemu ya sababu iliyomfanya Mwanagza kuokolewa.

Video hiyo iliyochezwa katika Seneti ilimshuhudia Mwangaza akitokwa na machozi alipokuwa akihojiwa na wakili wake.