Makanisa ya Kipentekoste yamekashifu hatua ya serikali ya kuongeza ada za usajili wa ndoa.
Muungano huo ulisema kuongezwa kwa ada hizo kutachochea upotovu wa maadili kwani vijana wengi watakwepa kusajili ndoa zao.
Mwenyekiti wa muungano wa makanisa hayo (CCAK) Hudson Ndeda alimsihi Rais William Ruto kutafakari upya na kurejelea uamuzi wake na baraza la mawaziri akisema Mkuu wa Nchi aliahidi kutumikia wakenya vyema.
“Kama kanisa, tuna wasiwasi zaidi kuhusu ongezeko la ada za usajili wa ndoa, bila shaka kanisa ni mdau mkuu katika eneo hili kwa vile tunawajibika kufunza mambo ya ndoa na kufungisha ndoa,” akasema.
Ndeda alisema wengi wa Wakenya tayari wanaishi chini ya mstari wa umaskini.
"Tuna wajibu wa kupiga tarumbeta kama vile Biblia inavyoamuru katika Ezekieli 33:3-5 wakati matatizo fulani ya kijamii na ukosefu wa haki yanapoachwa bila kudhibitiwa," aliongeza.
Alitaja ongezeko la ada za kufikia serikali kuwa sio haki na ni kinyume cha utu.
Serikali iliongeza tozo za usindikaji wa ndoa katika ofisi ya Mwanasheria Mkuu kutoka Sh5,000 hadi Sh50,000.
"Wanandoa wanaopambana na gharama ya juu ya maisha na wanaotaka kurasimisha ndoa zao katika ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali watalazimika kuchimba zaidi mifukoni mwao ikiwa ada mapya zitaanza kutumika,"alisema.
Mahakama Kuu imetoa maagizo ya muda ya kusitisha utekelezaji wa ada hizo mpya huku kesi ikitarajiwa kusikizwa.