Mshukiwa wa mauaji ya mke wa kakake na watoto 2 akamatwa Kisii

Mshukiwa aliingia kisiri nyumbani kwa nduguye akiwa na panga na kuwaua watatu hao.

Muhtasari

• Kulingana na polisi, majirani walisema kuwa mshukiwa alikuwa na maelewano na kaka yake kuhusu suala ambalo halijabainishwa.

Crime scene
Crime scene
Image: HISANI

Polisi mjini Kisii wamemkamata mwanamume mwenye umri wa miaka 27 aliyeripotiwa kumuua mke wa kaka yake na watoto wawili. Kulingana na ripoti ya polisi, mshukiwa alimuua mke wa kaka yake na watoto kutokana na ugomvi wa kifamilia siku ya Jumanne. 

Kisa hicho kilitokea katika kijiji cha Mesaria kaunti ya Kisii.Polisi walisema kuwa mwanamume huyo alikuwa ameenda mafichoni na alikamatwa Jumanne usiku katika lokesheni ya Kegogi, kaunti ndogo ya Marani.

 Kulingana na polisi, majirani walisema kuwa mshukiwa alikuwa na maelewano na kaka yake kuhusu suala ambalo halijabainishwa.

 "Muda mfupi kabla ya kumshambulia mke wa kakake mwenye umri wa miaka 27 na watoto wake wawili wenye umri wa miaka 4 na 3, majirani waliripoti kushuhudia makabiliano makali kati ya mshukiwa na kaka yake kuhusu suala ambalo halijabainishwa," taarifa ya polisi ilisema kwa sehemu. 

Ripoti ya polisi inaonyesha kwamba aliingia kisiri nyumbani kwa nduguye akiwa na panga na kuwaua watatu hao. Polisi walisema kuwa vikosi vya usalama vilianzisha msako na kumkamata mtuhumiwa kabla hajaenda mbali. 

Polisi wanaendelea na uchunguzi kabla ya kumfikisha mshukiwa kortini.