Seneta wa Nyeri Wahome Wamatinga asema lazima katibu mkuu wa UDA atoke Mlima Kenya

Seneta Wamatinga alisema DP Rigathi Gachagua atamuunga mkono Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro kwa wadhifa wa katibu mkuu.

Muhtasari

• Wamatinga alisema hata kabla ya  kuingia mamlakani utawala wa Kenya Kwanza kuingia mamlakani  William Ruto na Naibu na wake Rigathi Gachagua wangekuza viongozi vijana.

Katibu mkuu wa UDA Cleophas Malala
Katibu mkuu wa UDA Cleophas Malala
Image: Facebook

Seneta wa Nyeri Wahome Wamatinga amesisitiza kuwa Katibu Mkuu ajaye wa UDA anafaa kutoka Mlima Kenya.

Seneta huyo alisema kuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua atamuunga mkono Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro kwa wadhifa wa katibu mkuu.

"Ndindi ni kiongozi chipukizi na anaweza kuongoza na DP angemuunga mkono. Katika mkutano wetu tulisema lazima SG atoke Mlima Kenya," Wamatinga alisema.

Wamatinga alisema iko katika rekodi hata kabla ya utawala wa Kenya Kwanza kuingia mamlakani kwamba Rais William Ruto na Naibu wake Rigathi Gachagua wangekuza viongozi vijana.

Alisema hata Bungeni, kamati zinazoonekana kuwa na ushawishi walipewa viongozi vijana.

"Waliapa kwa sababu wanajua wanapoondoka afisini, wanataka kuwakabidhi vijana ambao wana uwezo wa kuongoza nchi hii ipasavyo," Seneta huyo alisema.

Mwezi Septemba, chama cha United Democratic Alliance cha Rais William Ruto kilifichua kile ambacho uongozi wake unaita mfumo wa thabiti ambao utawezesha wanachama wakipiga kura kwa njia ya kielektroniki katika chaguzi zijazo za chama.

Mkutano wa Baraza kuu la Kitaifa la chama hicho uliofanyika Septemba 29, uliamua kwamba baraza hilo liliazimia kuandaa uchaguzi huo tarehe 9 Desemba 2023.

Huu utakuwa uchaguzi wa kwanza kabisa wa chama hicho tangu kuanzishwa kwake 2021, lakini ndio uchaguzi muhimu zaidi kwani Rais Ruto anaweka msingi wa kugombea tena urais 2027.

Kabla ya uchaguzi wa chama cha UDA, Seneta wa Kakamega Boni Khalwale mwezi uliopita aliwasilisha ombi katika Kamati ya Kusuluhisha Mizozo ya chama hicho akitaka Katibu Mkuu Cleophas Malala aondolewe madarakani.

Katika maombi hayo, Khalwale na mwanachama mwingine wa UDA, Walter Mkinginyi Trenk, walimtuhumu Malala kwa kunyakuwa mamlaka ya Bodi ya kitaifa ya Uchaguzi ya chama hicho.

Walalamishi hao walikashifu hatua ya katibu mkuu kuteua wasimamizi wa kaunti na mikoa kusimamia uchaguzi ujao wa mashinani uliopangwa kufanyika Desemba 9.