logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Kesi ya Maina Njenga yatatizwa na fujo kufuatia uwepo wa polisi wengi

"Polisi wanamchukulia kila mtu kama mwanachama wa Mungiki na hatujui ni nini kilichangia  uamuzi wao," Njiru alisema.

image
na Davis Ojiambo

Habari21 November 2023 - 09:28

Muhtasari


  • • Wakili Ndegwa Njiru alisema ni makosa kwa polisi waliojihami kufunga barabara zote zinazoelekea katika Mahakama ya Sheria
  • • "Polisi wanamchukulia kila mtu kama mwanachama wa Mungiki na hatujui ni nini kilichangia  uamuzi wao,"
Maina Njenga wakati wa kusikilizwa kwa kesi dhidi yake Nakuru

Kesi dhidi ya Maina Njenga na wengine 11 ilikosa kuanza jinsi ilivyokuwa imeratibiwa baada ya timu ya utetezi kupinga uwepo wa polisi kwa wingi katika mahakama hiyo.

Wakili Ndegwa Njiru alisema ni makosa kwa polisi waliojihami kufunga barabara zote zinazoelekea katika Mahakama ya Nakuru kwa nia ya kuwazuia wananchi.

Alitishia kuwa upande wa utetezi utafanya maandamano ikiwa marafiki na jamaa wa washtakiwa 12 hawataruhusiwa kuhudhuria kikao cha mahakama akiongeza kuwa Kenya si taifa la polisi.

Alimwambia Hakimu Mkuu Kipkurui Kibelion kumwita Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Nakuru na kumwamuru kuwatoa maafisa hao wa  polisi karibu na Mahakama  ya Nakuru.

“Hata mawakili hawaruhusiwi kortini kabla ya kuonyesha vitambulisho ili kuthibitisha kuwa wao ni wanachama wa Chama cha Wanasheria wa Kenya,” alisema.

Maoni yake yaliungwa mkono na Mawakili Evanson Ondiek na Olaly Cheche waliosema umma una haki ya kushuhudia utekelezaji wa haki.

"Polisi wanamchukulia kila mtu kama mwanachama wa Mungiki na hatujui ni nini kilichangia  uamuzi wao," Ondiek alisema.

Aliishutumu Serikali kwa kutumia polisi kuwatisha watuhumiwa na jamaa zao.

Kiongozi wa mashtaka Wycliffe Omwenga alipuuzilia mbali maombi hayo kwa upande wa utetezi akisema kuwa mahakama hiyo ina uwezo wa kuwaruhusu watu wachache kuhudhuria vikao.

Alidai kuwa shahidi alizirai siku ya Jumatatu kutokana na msongamano katika chumba cha mahakama.

Hakimu Kibelion alibainisha kuwa ingawa mahakama haiwezi kuchukua kila mtu, upande wa mashtaka na upande wa utetezi unaweza kujadili nani wa kuruhusiwa kuingia.

Aliahirisha kesi hiyo kwa dakika 20 ili kuruhusu pande zinazopingana kukubaliana.

Njenga na washukiwa wenza wanashtakiwa kwa kuwa wanachama wa kundi lisilo halali, kuhudhuria mkutano haramu, kumiliki bunduki na bangi kinyume cha sheria na kusajili watu katika kundi haramu miongoni mwa mashataka mengine.

Makosa hayo yalidaiwa kutendeka kati ya Mei 11 na Mei 12 2023 katika eneo la Githioro eneo la Wanyororo katika Kaunti Ndogo ya Bahati.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved