4 zaidi wakamatwa kuhusiana na milioni 94.9 za Quickmart zilizoibiwa na wafanyikazi wa Wells Fargo

Washukiwa hao walikamatwa kwa madai ya kuzembea kazini na pia wanaaminika kula njama na washukiwa wawili wakuu

Muhtasari

•Wanne waliokamatwa ni wafanyikazi wa Wells Fargo, wenzao wa washukiwa wakuu wakuu wanaoaminika kutoroka na kiasi hicho kikubwa cha pesa.

•Kufikia sasa, washukiwa wanane wametiwa mbaroni kuhusiana na wizi huo na zaidi ya Sh 9 milioni tayari zimepatikana.

Pingu

Washukiwa wengine wanne walikamatwa Ijumaa kuhusiana na wizi wa Sh94.9 milioni za Quickmart Supermarket uliofanyika mapema mwezi huu.

Wanne waliokamatwa siku ya Ijumaa pia ni wafanyikazi wa Wells Fargo, wenzao wa washukiwa wakuu wawili wanaoaminika kutoroka na kiasi hicho kikubwa cha pesa mnamo Novemba 6. Wanne hao ni Joel Oyuchi Mweseli (Mdhibiti/Mpangaji), Harrison Mugendi Njeru (Afisa ambaye anasimamia madereva), Caleb Ouma Okinyi (Msimamizi wa Magari), na Ronald Ouma Oluu anayesimamia makamanda wa wafanyakazi.

Washukiwa hao walikamatwa kwa madai ya kuzembea kazini na pia wanaaminika kula njama na washukiwa wawili wakuu, Daniel Mugetha na Anthony Nduiki, ambao bado hawajapatikana. Sasa watakaa wikendi nzima chini ya ulinzi wa polisi na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani Jumatatu, Novemba 27.

Kufikia sasa, washukiwa wanane wametiwa mbaroni kwa tuhuma za wizi wa shilingi Sh94.9 milioni za Quickmart na zaidi ya Sh9 milioni tayari zimepatikana. Uchunguzi wa kuwasaka washukiwa zaidi wakiwemo washukiwa wawili wakuu bado unaendelea.

Siku chache zilizopita, washukiwa wengine wanne walikamatwa katika maeneo tofauti ndani na karibu na Nairobi baada ya kuhusishwa na uhalifu huo.

Takriban wiki mbili zilizopita, wapelelezi kutoka Kurugenzi ya Makosa ya Jinai (DCI)  ambao wanashughulikia kesi hiyo walifanikiwa kuwakamata washukiwa wanne.

Wanne hao walikamatwa katika maeneo tofauti baada ya kuhusishwa na wizi huo ambao ulishtua taifa zima mapema mwezi huu na. Ksh 9,101,300 zilipatikana kutokana na operesheni hiyo.

Kulingana na Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS), mshukiwa wa kwanza, Ismael Patrick Gitonga alikamatwa katika eneo la Rongai, Kaunti ya Kajiado baada ya kubainika kuwa gari lake aina ya Toyota Fielder lilitumiwa kubeba pesa zilizoibwa kutoka kwa gari la kusindikiza lililokuwa limezibeba.

Gitonga pia aliripotiwa kuwa ndiye aliyeendesha gari hilo baada ya kuchukua pesa hizo.

Washukiwa wengine wawili, Michael Matolo Njeru na Samwel Onyango walikamatwa katika eneo la Njiru, jijini Nairobi walipokuwa katika harakati za kulifanyia ukarabati gari linaloripotiwa kubeba pesa hizo, ili kuficha utambulisho wake.

Polisi waliripoti kwamba mshukiwa wa nne, Martin Nderi Nganga alikamatwa katika mtaa wa Kasarani, Nairobi na Ksh9,101,300 zilipatikana katika nyumba yake ya kukodi.

"Pia iliyopatikana ni sanduku la pesa kwenye msitu karibu na Soko la Gataka, katika mtaa wa Karen," NPS ilisema katika taarifa Jumapili asubuhi.

Wakati huo , Maafisa wa upelelezi wanaoshughulikia kesi hiyo ya wizi walitangaza kwamba wangeendelea na msako wa kutafuta pesa zilizosalia zilizoibwa na kuwakamata washukiwa wengine zaidi.