Mlinzi wa nyumbani wa Kalonzo afariki akidaiwa kunywa sumu

Haijabainika ni kwa muda gani afisa huyo alikuwa akifanya kazi katika nyumba ya Kalonzo

Muhtasari

•Jumapili wenzake walimsikia akilia kwa maumivu ndani ya nyumba yake katika boma la Kalonzo na kuharakisha kujua kilichokuwa kikiendelea

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, ambaye alipoteza mlinzi katika nyumba yake kijijini Tseikuru huko Kitui Picha: MUSEMBI NZENGU
Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, ambaye alipoteza mlinzi katika nyumba yake kijijini Tseikuru huko Kitui Picha: MUSEMBI NZENGU

Polisi mjini Kitui wanachunguza kifo cha afisa wa polisi aliyepewa jukumu la kulinda nyumba ya  kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka.

Siku ya Jumatatu, kamanda wa polisi kaunti ya Kitui Leah Kithei alisema polisi huyo alisemekana kujitoa uhai kwa kunywa sumu.

Akizungumza katika afisi yake mjini Kitui, Kithei alisema kuwa mwendo wa saa nane unusu siku ya Jumapili wenzake walimsikia akiwa katika maumivu ndani ya nyumba yake katika boma la Kalonzo na kuharakisha kujua kilichokuwa kikiendelea.

"Walimpata amelala bila fahamu kwenye kitanda chake na kumkimbiza katika Hospitali ya Mumoni Nursing iliyo karibu na kituo cha biashara cha Tseikuru ambako alifariki alipokuwa akipewa matibabu," Kithei alisema.

Alisema kuwa  hakuweza kutaja utambulisho wa afisa huyo ambaye kwa sababu hakuwa na uhakika kama jamaa zake wa karibu walikuwa wamefahamishwa kuhusu kifo chake.

"Ninachoweza kusema ni kwamba tumeanza uchunguzi kuhusu kifo hicho, Wacha tusubiri hadi mwisho wa uchunguzi ikiwa ni pamoja na uchunguzi wa maiti ili ukweli ujulikane," Kithei alisema.

Haijabainika ni kwa muda gani afisa huyo alikuwa akifanya kazi katika nyumba ya mashambani ya Kalonzo kwani gazeti la The Star ,halikuweza kumfikia kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Tseikuru Fredrick Onyango ili atoe maoni yake. Onyango alisemekana kuwa hayuko likizoni.