Polisi wa trafiki wamepigwa marufuku kubeba bunduki wakiwa kazini

Hayo yanajiri baada ya maafisa watatu wa trafiki kufyatulia risasi Maafisa wa upelelezi wa EACC

Muhtasari

•Maafisa wa upelelezi wa EACC Alhamisi waliwakamata maafisa watatu wa polisi wa trafiki kwa kuitisha hongo katika Barabara ya Naivasha-Mai Mahiu


Mchoro wa afisa wa trafiki
Mchoro wa afisa wa trafiki

Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi Mirriam Muli alitangaza kupigwa marufuku kwa maafisa wa trafiki kubeba bunduki kazini kupitia taarifa iliyotumwa kwa wakuu wote wa polisi wa mikoa kote nchini.

"Imebainika kwa waziwazi  kwamba maafisa wanaohusika kikamilifu na majukumu ya trafiki wana silaha,Hii imesababisha matumizi mabaya ya silaha kwa maafisa hao Kuanzia sasa hakuna afisa anayehusika na trafiki atakayebeba bunduki," ilisema taarifa hio.

Aliongeza zaidi kuwa Makamanda wote  wanapaswa kuhakikisha kuwa agizo hili linazingatiwa mara moja.

Maagizo hayo yalitolewa baada ya mkuu wa EACC Twalib Mbarak kumtaka Inspekta Jenerali wa Polisi Japhet Koome kuwapokonya silaha maafisa wote wa polisi wa trafiki kote nchini kwa madai kuwa baadhi ya maafisa wa polisi wa trafiki wanatumia bunduki za serikali kukabiliana na maafisa wa upelelezi wa EACC wanaponaswa wakidai rushwa barabarani.

Maafisa wa upelelezi wa EACC Alhamisi waliwakamata maafisa watatu wa polisi wa trafiki kwa kuitisha hongo katika Barabara ya Naivasha-Mai Mahiu.

Maafisa hao watatu, Koplo James Njeru na Konstebo wa Polisi Dickson Njagi na James Mwai wanasemekana kuomba Ksh.15,000 kutoka kwa madereva saa moja kabla ya kukamatwa kwao, ambayo waliwaona polisi hao wahalifu wakifyatua risasi hewani kabla ya kutiishwa.