Afisa wa polisi akamatwa na wapelelezi wa EACC kwa kudai hongo ili kuwaachilia washukiwa wawili

Mshukiwa, Paul Kamau Mbugua, alikamatwa katika duka la kuuza vileo kando ya barabara ya Lumumba Driv

Muhtasari
  • Akithibitisha kukamatwa kwa mshukiwa huyo, Msemaji wa EACC Eric Ngumbi alibainisha kuwa Tume ilipokea malalamishi kuhusu afisa huyo siku ya Ijumaa
Mwanaume aliyekamatwa
Mwanaume aliyekamatwa
Image: Sagwe

Maafisa wa upelelezi kutoka Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) Ijumaa walimkamata afisa wa polisi wa Kasarani kwa kuitisha hongo ya Ksh.30,000.

Mshukiwa, Paul Kamau Mbugua, alikamatwa katika duka la kuuza vileo kando ya barabara ya Lumumba Drive kwa kudai hongo hiyo ili kuwaachilia ndugu wawili aliowakamata kimakosa na kuwazuilia katika Kituo cha Polisi cha Kasarani.

Mbugua, EACC inasema, hakuandika makosa ya ndugu hao katika kitabu cha matukio ya kituo hicho.

Licha ya kukataa kukamatwa na kusababisha tukio katika duka hilo la vileo, makachero wa EACC walifanikiwa kumkamata mshukiwa  na kumpeleka katika Kituo cha Polisi cha Kilimani.

"Mshukiwa alisindikizwa hadi katika Kituo cha Polisi cha Kilimani ambako anazuiliwa kwa sasa akisubiri kushughulikiwa zaidi leo katika Kituo cha Polisi cha EACC Integrity Center," chanzo katika shirika la kupambana na ufisadi kiliambia Citizen Digital.

"Wapelelezi walimnyang'anya mshukiwa bunduki aina ya Taurus Revolver Pistol S/No. Q130360 na risasi, ambazo baadaye walikabidhi kwa Kituo cha Polisi cha OCS EACC."

Akithibitisha kukamatwa kwa mshukiwa huyo, Msemaji wa EACC Eric Ngumbi alibainisha kuwa Tume ilipokea malalamishi kuhusu afisa huyo siku ya Ijumaa, na baadaye kufanya uchunguzi na kumkamata mshukiwa.