11 wathibitishwa kufariki katika ajali mbaya iliyotokea katika barabara kuu ya Kisumu-Nairobi

"Tunaweza kusema kwa sasa karibu watu 10 wamekufa, mtoto ambaye ana umri wa miaka 3 hadi 4 alikufa," polisi walisema.

Muhtasari

•Kulingana na kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Nyando Grace Thuo, ajali hiyo ilihusisha basi la Super Metro na lori.

•Thuo alibainisha kuwa huenda idadi hiyo ikaongezeka kwa sababu kulikuwa na watu waliopata majeraha tofauti.

Gari la Super Metro Bus likiondolewa kutoka eneo la ajali eneo la Otho huko Kisumu
Gari la Super Metro Bus likiondolewa kutoka eneo la ajali eneo la Otho huko Kisumu
Image: FAITH MATETE

Zaidi ya watu 10 wamethibitishwa kufariki akiwemo mtoto kufuatia ajali mbaya ya barabarani iliyotokea katika eneo la Othoo huko Awasi kando ya barabara kuu ya Kisumu Nairobi.

Kulingana na kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Nyando Grace Thuo, ajali hiyo ilihusisha basi la Super Metro na lori.

Basi hilo lilikuwa likielekea Nairobi kutoka Kampala.

Thuo alibainisha kuwa ajali hiyo ilitokea wakati dereva wa basi hilo alipokuwa akijaribu kupita.

"Magari yote mawili yameharibika na tunaweza kusema kwa sasa karibu watu 10 wamekufa, mtoto ambaye ana umri wa miaka 3 hadi 4 alikufa," Thuo alisema.

Alibainisha kuwa huenda idadi hiyo ikaongezeka kwa sababu watu kadhaa ambao walikimbizwa katika hospitali mbalimbali walikuwa na majeraha tofauti.

Mmoja wa maafisa wa Msalaba Mwekundu karibu na eneo hilo ambaye aliarifu Radio Jambo kuhusu kisa hicho alibainisha kuwa ajali hiyo ilitokea mwendo wa saa nane usiku wa kuamkia Jumatatu.

“Ajali hii ni mbaya, naona maiti kadhaa hapa, basi liligongana na lori lililokuwa limebeba mchele kwa sababu tuliona limetawanyika kila mahali,” alisema.

Mwandishi wa habari ambaye alikusudiwa kuwa ndani ya basi hilo lakini akaikosa alichapisha kwenye kundi moja akimshukuru Mungu kwa kuokoa maisha yake.

“Namshukuru Mungu sana kwa sababu nilipanga basi kutoka Kisumu, siwezi kusema kilichotokea kwa sababu abiria wengine ambao tulikuwa tumepanga nao walipanda huku mimi nikiwakosa,” alisema.