Gavana Wavinya aagiza kuchunguzwa kwa dhulma dhidi ya MCA

Gavana huyo aliagiza Katibu wa Kaunti na Mkuu wa Utumishi wa Umma kuanzisha uchunguzi mara moja kuhusu madai hayo.

Muhtasari

• Maeke alikataa kukamatwa na maafisa hao kabla ya baadhi ya wafanyakazi wenzake na wananchi kuingilia kati.

MCA wa Kalama Boniface Maeke akishambuliwa na askari wa Kaunti ya Machakos katika Mahakama ya Sheria ya Machakos mnamo Januari 31, 2024. Picha: HISANI
MCA wa Kalama Boniface Maeke akishambuliwa na askari wa Kaunti ya Machakos katika Mahakama ya Sheria ya Machakos mnamo Januari 31, 2024. Picha: HISANI

Gavana wa Machakos Wavinya Ndeti ameagiza uchunguzi wa haraka ufanyike kuhusiana na madai ya kushambuliwa na kudhulumiwa kwa mwakilishi wa wadi na askari wa kaunti. 

Hii ilikuwa baada ya baadhi ya askari wa kaunti kukamatwa siku ya Jumatano kwa madai ya kumshambulia MCA wa Kalama Boniface Maeke ndani ya majengo ya mahakama. Askari hao wa kaunti walitiwa mbaroni baada ya afisa wa mahakama kumpigia simu afisa mkuu wa polisi katika kaunti hiyo na kusema kuwa mahakama ilikuwa ikishambuliwa. 

Maeke alikataa kukamatwa na maafisa hao kabla ya baadhi ya wafanyakazi wenzake na wananchi kuingilia kati. Askari wa kaunti walijaribu kumkamata MCA wa Kalama bila kufaulu katika majengo ya Mahakama mjini Machakos.

Katika taarifa, Ndeti alikashifu mashambulizi kutoka kwa maafisa wake akibainisha kuwa wafanyikazi wake wa utawala wanatarajiwa kufuata sheria.

 "Nakashifu vikali na udhalilishaji uliofanyiwa viongozi. Napenda kusisitiza dhamira ya uongozi wangu ya kuzingatia utawala wa sheria na kuheshimu haki za watu wote wakiwemo viongozi wetu," alisema. 

Gavana huyo aliagiza Katibu wa Kaunti na Mkuu wa Utumishi wa Umma kuanzisha uchunguzi mara moja kuhusu madai hayo.Ndeti alisema kuwa hatua zinazofaa za kiutawala zitachukuliwa dhidi ya watu ambao watapatikana na hatia. 

“Kwa kuzingatia hayo, natarajia ripoti itatumwa ofisini kwangu ndani ya siku 7 kuanzia leo (Jumatano),” aliongeza. 

Aidha, gavana huyo alitoa wito kwa maafisa wote wa usimamizi wa kaunti kuzingatia sheria na utaratibu wakati wote.Maafisa hao aidha wamehimizwa kuheshimu haki za wakaazi wote wa kaunti hiyo katika kutekeleza majukumu yao kwani imekuwa desturi watu wa kaunti hiyo. 

"Ninazidi kusema kuwa utawala wangu hautaunga mkono kitendo chochote cha ukiukaji sheria kinachofanywa na wafanyikazi wa kaunti kwa wakaazi," Ndeti aliongeza. 

Katika kisa cha Jumatano, wafanyikazi wa kaunti waliokamatwa walielekezwa kurekodi taarifa katika kituo cha polisi cha Machakos DCI. MCA Maeke alirekodi taarifa yake katika kituo hicho kabla ya kupelekwa hospitalini kwa matibabu.

Akizungumza kwa njia ya simu saa chache baadaye, MCA huyo alidai kuwa alivuliwa nguo na wavamizi wake wakati wa kisa hicho. 

"Sijui ni kwa nini walinishambulia. Najua baadhi ya washambuliaji wangu, wanafanya kazi katika Serikali ya Kaunti ya Machakos kama maafisa wa ukaguzi," Maeke alisema.

Alisema alikuwa ameandamana na mwenzake wa Masii/Vyulya Douglas Musyoka kortini aliposhambuliwa. Askari wa kaunti ya Machakos waliripotiwa kumkamata Musyoka siku ya Jumanne. Alishtakiwa kwa kujenga nyumba bila idhini muhimu kutoka kwa kaunti.

MCA aliachiliwa kwa dhamana ya Shilingi 50,000 pesa taslimu.Maeke alisema hakujua kwa nini alishambuliwa. Alisema alitafuta matibabu katika hospitali ya Machakos kutokana na majeraha aliyoyapata kwenye mguu na mkono.

 "Gari lilijeruhi mguu wangu mmoja wakati wa tukio. Ninaendelea vyema na matibabu," Maeke alisema.