logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Kifo cha Moi, makachero warejea kwa Khalwale kuchimbua zaidi

Mwili wa Moi ulipatikana siku ya Jumapili ndani ya zizi la ng'ombe.

image
na Davis Ojiambo

Habari01 February 2024 - 14:27

Muhtasari


  • • Siku ya Jumatano, mbunge huyo alisema yuko tayari kushirikiana na maafisa wa upelelezi ili kuondoa shauku yoyote.
  • • Hii ni baada ya baadhi ya watu kudai kulikuwa na zaidi kuhusu kifo cha Moi kuliko inavyoonekana.
  • • Khalwale alisema Moi aliuawa kwa kushambuliwa na fahali wake wa kupigana aliyekuwa akichunga.
akiwahutubia wanahabari baada ya fahali wake kumuua mfanyikazi wake siku ya Jumamosi, Januari 27, 2024.

Maafisa wa upelelezi Alhamisi walitembelea boma la Seneta wa Kakamega Boni Khalwale la Malinya kwa siku ya pili mfululizo ili kuendeleza uchunguzi kuhusu kifo cha mfanyikazi wake wa muda mrefu Kizito Moi.

Mwili wa Moi ulipatikana siku ya Jumapili ndani ya zizi la ng'ombe katika kile ambacho seneta huyo alidai aliuawa kwa kushambuliwa na fahali wake wa kupigana aliyekuwa akichunga.

"Siku ya tatu ya uchunguzi wa kifo cha ghafla cha mlinzi wangu wa fahali wa kupigana. Makachero walirudi leo. Ninamshukuru Bw. Martin Nyundi kutoka idara ya kitaifa ya mauaji kwa hakikisho kwamba hakuna kinachoachwa cha kutiliwa shaka,” Khalwale alisema katika ujumbe wa kwa X.

Siku ya Jumatano, mbunge huyo alisema yuko tayari kushirikiana na maafisa wa upelelezi ili kuondoa shauku yoyote baada ya baadhi ya watu kudai kulikuwa na zaidi kuhusu kifo cha Moi kuliko inavyoonekana.

Alikanusha madai yaliyoenea kwenye mitandao ya kijamii kwamba alihusika katika kifo cha mfanyikazi wake wa muda mrefu.

"Nimefungua nyumba yangu kwa polisi ili kuwapa fursa ya kufanya uchunguzi wa kuaminika na wa suluhu kuhusu kifo hiki cha kusikitisha na hivyo kuwawezesha kufuatilia suala hilo kwa hitimisho la kimantiki kabla ya mipango ya mazishi kuendelea," Seneta huyo alisema.

“Watu ambao wamesema hivyo ni akina nani? Wewe ni mwanahabari...unamwomba seneta wa Kakamega kufafanua masuala kwenye mitandao ya kijamii,” aliambia Star kwenye simu alipofikiwa ili atoe maoni yake.

Khalwale alisema atatangaza kila kukicha uchunguzi unaoendelea kwa sababu hana la kuficha. Mwili wa Kizito ulikuwa na majeraha mengi yanayoaminika kusababishwa na fahali huyo.

Uchunguzi wa mwili wake unatarajiwa kufanyika katika hospitali kuu ya kaunti ya Kakamega. Khalwale alimuua fahali huyo kwa jina ‘Inasio’ siku ya Jumapili kwa kile alichosema ni kwa kuzingatia utamaduni wa Waluhya.

Seneta huyo alisema Jumatano alisema waliahirisha mazishi ya Kizito hadi polisi watakapobaini ukweli kuhusu tuhuma zinazotolewa dhidi yake na "wanasiasa bandia".

Moi, 47, amekuwa mfanyikazi wa Khalwale kwa zaidi ya miaka 20. "Alikuja hapa akiwa mvulana mdogo," Khalwale alisema katika mahojiano Jumapili.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved