Wanafunzi wa Multimedia waandamana baada ya mmoja wao kushambuliwa na fisi

Mwanafunzi huyo wa mwaka wa pili alishambuliwa Jumatatu usiku mwendo wa saa mbili usiku.

Muhtasari

•Kelvin Mwenda mwenye umri wa miaka 21, mwanafunzi wa mwaka wa pili, alishambuliwa Jumatatu usiku mwendo wa saa mbili usiku.

•Kiongozi wa KUSO amehimiza Shirika la Huduma ya Wanyamapori (KWS) kuchukua hatua kwa usalama wa wanafunzi.

waliandamana Jumanne asubuhi
Wanafunzi wa Multimedia waliandamana Jumanne asubuhi
Image: SCREENGRAB

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Multimedia mnamo siku ya Jumanne walijitosa barabarani kuandamana baada ya mmoja wao kushambuliwa na fisi.

Kelvin Mwenda mwenye umri wa miaka 21, mwanafunzi wa mwaka wa pili, alishambuliwa Jumatatu usiku mwendo wa saa mbili usiku.

Taasisi hiyo ya elimu ya juu iko mkabala na Hifadhi ya Kitaifa ya Nairobi.

Kiongozi wa Miungano ya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu vya Kenya Jesse Saruni alisema mwanafunzi huyo alipoteza kidole gumba kimoja wakati wa shambulio hilo.

"Alikuwa akitoka shuleni akielekea nyumbani kwake Rongai mwendo wa saa mbili usiku wakati kisa hicho kilitokea. Fisi pia aling'ata upande mmoja wa uso wake," Saruni alisema.

"Jicho lake limefunikwa. Hatuna uhakika kama jicho lake lingine liko sawa kwa sababu amefunikwa upande mmoja wa uso," Saruni alisema.

Kiongozi huyo wa wanafunzi alihimiza Shirika la Huduma ya Wanyamapori (KWS) kuchukua hatua kwa usalama wa wanafunzi.

"Hamuwezi kulala kazini huku wenzetu wakidhulumiwa na fisi kushoto kulia na katikati," Rais wa KUSO alisema.

"Kama kazi imewashinda tutaunda kikosi kazi cha kuzungumza na fisi kama mlivyoshauri. Tutazungumza nao kwa lugha watakayoielewa."

Ripoti ya polisi kutoka Olekasasi ilionyesha mwanafunzi huyo alishambuliwa kando ya barabara ya Maasai Lodge.

"Stephen Romo, ambaye ni mkazi wa kijiji hiki, alikimbia kumuokoa na kupata majeraha mabaya sana. Wawili hao kwa sasa wako katika Hospitali ya Wama Nursing Home wakipokea matibabu," polisi walisema.