Dennis Itumbi asherehekea baada ya Jacque Maribe kuondolewa mashtaka ya mauaji

Itumbi amebainisha kuwa hajutii kusimama na Bi Maribe katika kipindi chote cha kesi hiyo iliyochukua miaka sita.

Muhtasari

•Itumbi alisema anahisi amethibitishwa kuwa sahihi baada ya mashtaka yote dhidi ya mwanahabari huyo wa zamani kuondolewa.

•Mwanablogu huyo pia alitumia fursa hiyo kumtia moyo Bi Maribe kujitahidi kuinuka tena baada ya yale ambayo amepitia.

akimsindikiza Jacque Maribe nje ya Mahakama ya Milimani mnamo Februari 9, 2024.
Dennis Itumbi akimsindikiza Jacque Maribe nje ya Mahakama ya Milimani mnamo Februari 9, 2024.
Image: DOUGLAS OKIDDY

Muda mfupi tu baada ya rafiki yake mkubwa Jacque Maribe kuondolewa mashtaka katika kesi ya mauaji ya mfanyibiashara Monica Kimani, mtaalamu wa mikakati ya kidijitali Dennis Itumbi aliandika taarifa ndefu kusherehekea uamuzi wa mahakama.

Katika taarifa yake Ijumaa adhuhuri, Itumbi alisema anahisi amethibitishwa kuwa sahihi baada ya mashtaka yote dhidi ya mwanahabari huyo wa zamani kuondolewa.

Alisisitiza kuwa Maribe hakumuua marehemu mfanyabiashara huyo mwaka wa 2018 na akamshtumu mkuu wa upelelezi wa zamani kwa kumburuta hadi kwenye kesi hiyo.

“Jacque Maribe yuko HURU! Maribe HAKUMUUA Monica. Daaamn! Ninahisi kuthibitishwa sahihi!,” Itumbi aliandika kwenye mtandao wa Facebook.

Aliongeza, "Imekuwa miaka SITA, safari ya vivuli, ambapo minyororo isiyo ya haki ilitafuta kufunga roho ya rafiki mkubwa, haiba ya kupendeza, rafiki ninayemthamini sana. Leo, ukweli umefichua mwangaza wake, ukiondoa giza.

Mwanablogu huyo pia alitumia fursa hiyo kumtia moyo Bi Maribe kujitahidi kuinuka tena baada ya yale ambayo amepitia katika miaka sita iliyopita tangu kesi hiyo kuanza.

"Kama marafiki zako, mikono yetu ya pamoja inanyooshwa kukushikilia unapochukua hatua zinazofuata. Rafiki yangu mzuri, Karibu tena katika kukumbatia uhuru,” aliandika.

"Acha rekodi ionyeshe kuwa umekuwa HAUNA HATIA siku zote. Mfumo umeshindwa wewe na watu wahuni waliokuongeza katika kesi hii kwa vichwa vya habari na kuunda sarakasi wanapaswa kujibu na usiruhusu watoke nje ya fujo bila maswali, "aliongeza.

Itumbi pia alibainisha kuwa hajutii kusimama na wa mama huyo wa mvulana mmoja katika kipindi chote cha kesi hiyo iliyochukua miaka sita.

“Kwa familia ya Monica, zaidi ya Haki, Faraja ijaze mioyo yenu. Jacqueline Maribe, kuna sababu dhoruba zimepewa majina ya wanawake

Dhoruba, kama wanawake waliozingatia haziwezi kusimamishwa, wewe ni dhoruba nzuri! Ubarikiwe,” mwanablogu huyo aliandika.

Mtaalamu huyo wa mikakati wa kidijitali alikuwepo mahakamani wakati hukumu ya kesi ya mauaji ya Monica Kimani ilipokuwa ikitolewa Ijumaa. Alionekana akishiriki mazungumzo na kusherehekea pamoja na Bi Maribe mara baada ya kikao hicho cha mahakama kukamilika na ikaamuliwa hana hatia.