Familia ya Kakamega yajawa majonzi baada ya ndugu wawili kufariki katika mzozo wa miti

Ndugu hao walianza kupigania haki ya kukata miti kwenye ardhi iliyoachwa na marehemu baba yao.

Muhtasari

•Kisa hicho ambacho kilitokea katika kijiji cha Eregi, Ikolomani Mashariki pia kiliwaacha wengine kadhaa wakiwa wamejeruhiwa, akiwemo afisa wa polisi.

•Seneta wa Kakamega Boni Khalwale alisema kwenye taarifa kupitia X kwamba anaifahamu familia hiyo kibinafsi.

Wakaazi wakusanyika kuzunguka nyumba katika kijiji cha Eregi, Kaunti ya Kakamega baada ya vita vya miti kuzuka, Jumamosi, Februari 10, 2024.
Wakaazi wakusanyika kuzunguka nyumba katika kijiji cha Eregi, Kaunti ya Kakamega baada ya vita vya miti kuzuka, Jumamosi, Februari 10, 2024.
Image: HISANI

Familia moja katika Kaunti ya Kakamega imeingia katika maombolezo baada ya ndugu wawili kufariki siku ya Jumamosi katika mzozo wa miti.

Kisa hicho ambacho kilitokea katika kijiji cha Eregi, Ikolomani Mashariki pia kiliwaacha wengine kadhaa wakiwa wamejeruhiwa, akiwemo afisa wa polisi.

Wakazi na wanafamilia walisema ndugu hao walianza kupigania haki ya kukata miti kwenye ardhi iliyoachwa na marehemu baba yao.

Walisema polisi wakijibu mzozo uliofuata walifyatua risasi kadhaa, na wakati kila kitu kiliponyamaza, ndugu hao wawili walikuwa wamekufa.

“Walikuja mbio na kuingia nyumbani kwangu, mmoja alikuwa ameshika panga na akaanza kumkata dada yao,” jirani mmoja alisema.

"Milio ya risasi ilisikika, sijui zilimpata aje mume wangu. Waliendelea kwa muda," mjane wa mmoja wa marehemu alisema.

Seneta wa Kakamega Boni Khalwale alisema kwenye taarifa kupitia X kwamba anaifahamu familia hiyo kibinafsi.

Alisema mmiliki wa shamba hilo marehemu Mzee Shisanya Angote alimuuzia sehemu yake baada ya kuigawanya na kuwagawia watoto wake wa kiume na wa kike.

Seneta huyo alisema alijenga polytechnic kwenye ardhi aliyonunua kutoka kwa mzee huyo baada ya kugawanywa.

“Inasikitisha sana kwamba wanawe wawili wamepoteza maisha huku wakiingilia kile ambacho baba yao alimpa dada yao, Madam Maureen Bunoro Shisany,” alisema.

Seneta huyo aliwatakia waliojeruhiwa katika ajali hiyo ahueni ya haraka na kuwataka wakazi na familia kudumisha amani huku vyombo vya usalama vikijitahidi kurejesha utulivu.