Mshukiwa wa mauaji afariki baada ya kudaiwa kujitoa uhai katika seli ya polisi Nyeri

Ben Kamau Maina alikuwa akizuiliwa katika kituo hicho akisubiri kesi ya mauaji ya mkewe Nancy Muthoni Maina.

Muhtasari

•Mshukiwa wa mauaji alipatikana akiwa amefariki katika seli baada ya mshukiwa wa kudaiwa kujitoa uhai katika kituo cha polisi cha Mukurweini, Nyeri.

•Washukiwa wengine walisema walikuta maiti ya Maina ikiwa imening'inia kwenye sehemu ya dirishani huku kamba ya godoro ikiwa imefungwa shingoni.

Image: HISANI

Polisi na Mamlaka Huru ya Uangalizi wa Polisi (IPOA) wanachunguza kisa ambapo mshukiwa wa mauaji alipatikana akiwa amefariki katika seli baada ya mshukiwa wa kudaiwa kujitoa uhai katika kituo cha polisi cha Mukurweini, Nyeri.

Ben Kamau Maina alikuwa akizuiliwa katika kituo hicho akisubiri kesi ya mauaji ya mkewe Nancy Muthoni Maina, polisi walisema.

Kisa hicho kilitokea siku ya Jumatatu asubuhi alipokuwa amepangwa kufika mahakamani.

Polisi walisema alipangwa kufika katika mahakama ya eneo hilo kuhusu mauaji hayo.

Washukiwa wengine walioshikiliwa katika kituo hicho walisema walikuta maiti ya Maina ikiwa imening'inia kwenye sehemu ya dirishani huku kamba ya godoro ikiwa imefungwa shingoni mwake.

Alikuwa amefariki saa kadhaa awali. Washukiwa wengine waliwaarifu polisi waliokuwa zamu ambao walikimbilia eneo la tukio na kujaribu kumsaidia bila mafanikio.

Mwili huo ulihamishwa hadi katika chumba cha kuhifadhia maiti cha eneo hilo ukisubiri uchunguzi wa maiti.

Polisi walisema hawajabaini nia ya tukio hilo. Hakuwa amefichua kwa mtu yeyote juu ya mipango yake.

Kesi kama hizo huchunguzwa na IPOA.

Timu hiyo ilitembelea kituo hicho na kuzungumza na mashahidi wengine na polisi waliokuwa zamu kama sehemu ya upelelezi wa tukio hilo.