Maafisa wawili wa polisi wakamatwa Busia kwa madai ya wizi wa Sh2 milioni

Polisi walidai kupata shilingi 500,00 kwa gari walilokamata lakini wenye gari walisema lilikuwa na 2,600,00.

Muhtasari

• Wamiliki wa pesa hizo, hata hivyo, walilalamika kuwa pesa zilizotangazwa katika kituo cha polisi sio kiasi ambacho kilikuwa kwenye gari kabla ya kupelekwa kituoni.

Bunduki
Bunduki
Image: Andrew Kasuku

Maafisa wawili wa polisi wametiwa nguvuni mjini Busia kwa madai ya wizi wa Sh2 milioni.

Ripoti ya polisi iliyowasilishwa katika kituo cha polisi cha Busia na kufikia chumba chetu cha habari ilisema kuwa maafisa hao wawili na raia mmoja walikamatwa kuhusiana na wizi wa pesa hizo.

Polisi katika ripoti hiyo walisema kisa hicho kilitokea katika eneo la kuegesha magari katika hoteli moja mjini Busia mnamo Februari 25.

Pesa zilizopotea, polisi walisema, zilikuwa za Shirika moja la Kijamii.

"Hii ilitokea wakati maafisa [waliokamatwa] walipopata taarifa kwamba kulikuwa na watu wanaotiliwa shaka ambao walikuwa wakitafuta kubadilisha fedha kutoka shilingi za Kenya hadi shilingi za Uganda," sehemu ya ripoti ya polisi ilieleza.

"Maafisa hao wawili walijibu na kupata wanaume wanne ndani ya gari wakiwa na pesa taslimu Sh500,000."

"Dereva alijaribu kuvutana nao na maafisa wakaitisha nguvu zaidi na gari likapelekwa katika kituo cha polisi huku waliokuwamo [pia] wakipelekwa kituo cha polisi. Pesa zilizopatikana zilirekodiwa."

Polisi walisema baadaye raia wawili wa Kijerumani waliibuka wakidai pesa hizo ni zao kwa kuwa walikuwa wakifanya kazi katika shirika hilo la kijamii.

Wawili hao, hata hivyo, walilalamika kuwa pesa zilizotangazwa katika kituo cha polisi sio kiasi ambacho kilikuwa kwenye gari kabla ya kupelekwa kituoni.

Wanandoa hao walidai pesa hizo zilipaswa kuwa Sh2,600,000 na sio Sh500,000 zilizoandikwa katika kituo cha polisi.

Maafisa wa DCI wa kaunti wanachunguza tukio hilo.