Kenya na Haiti zasaini mkataba wa kutuma maafisa 1,000 wa polisi Caribbean

Waziri Mkuu wa Haiti aliwasili nchini Alhamisi, baada ya mwaliko kutoka kwa Rais William Ruto

Muhtasari
  • Makubaliano hayo yalitiwa saini Ijumaa, Machi 1, na Waziri wa Mambo ya Ndani (CS) Kithure Kindiki na Waziri wa Usalama wa Haiti katika Ikulu.
Kenya na Haiti zasaini mkataba wa kutuma maafisa 1,000 wa polisi
Image: PCS

Kenya na Haiti zimetia saini mkataba wa kutuma  maafisa wa polisi 1,000 katika nchi ya Carribean.

Makubaliano hayo yalitiwa saini Ijumaa, Machi 1, na Waziri wa Mambo ya Ndani (CS) Kithure Kindiki na Waziri wa Usalama wa Haiti katika Ikulu.

Pia walikuwepo Rais William Ruto na Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry.

Makubaliano hayo yanakuja licha ya amri ya mahakama iliyozuia mpango huo wa kupeleka wanajeshi, na kuutaja kuwa ni kinyume cha katiba.

Waziri Mkuu wa Haiti aliwasili nchini Alhamisi, baada ya mwaliko kutoka kwa Rais William Ruto, ambao alisema ulikuwa wa kukamilisha makubaliano kati ya mataifa hayo mawili kutuma wanajeshi wa Kenya katika nchi hiyo iliyokumbwa na machafuko.

Katika mkutano huo uliofanyika katika ikulu ya serikali, Ruto aliahidi kuisaidia Haiti kutatua tatizo la magenge katika taifa hilo la Caribean, kwani nchi hizo mbili zina asili moja.

"Tunatoa tajriba na utaalam wa maafisa wetu wa polisi katika Ujumbe wa Kimataifa wa Usaidizi wa Usalama wa Kimataifa nchini Haiti kama ilivyoagizwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kama inavyoongozwa na mahakama zetu," Ruto alisema.

Haya yanajiri baada ya genge la majambazi kufanya shambulizi, likizingira uwanja mkuu wa ndege wa Haiti, mashirika ya serikali na vituo vya polisi, ambalo lililemaza operesheni nchini humo mnamo Alhamisi, Februari 29.

Mnamo Januari 26, Mahakama Kuu ya Nairobi kupitia uamuzi uliotolewa na Jaji Chacha Mwita ilitangaza kutumwa kwa polisi nchini Haiti kinyume na katiba, na kuongeza kuwa Polisi wa Usalama wa Kitaifa hawawezi kupeleka maafisa wa polisi nje ya nchi.