Mhusika mkuu wa mauaji ya mfanyibiashara Monica Irungu, Joseph Irungu almaarufu Jowie atajua hatima yake siku ya Jumatano wiki ijayo, Machi 13, baada ya mahakama kuahirisha hukumu yake siku ya Ijumaa.
Jaji Grace Nzioka ambaye amekuwa akishughulikia kesi hiyo nzito alitoa uamuzi huo baada ya kubaini kuwa stakabadhi muhimu ambazo zingeweza kusaidia mahakama kufikia uamuzi wake wa mwisho ziliwasilishwa kwa kuchelewa.
Mahakama Kuu ilitarajiwa kutoa hukumu yake dhidi ya Jowie siku ya Ijumaa, Machi 8, baada ya kupatikana na hatia ya mauaji ya Monica.
Hii ni baada ya kupatikana na hatia ya mauaji katika uamuzi uliotolewa na Jaji Grace Nzioka mnamo Februari 9, na kuhitimisha kesi ya mauaji iliyoanza mwaka wa 2018.
Mahakama ya Nairobi iliamua kwamba upande wa mashtaka ulitoa ushahidi wa kutosha na kuthibitisha bila shaka kwamba Jowie alimuua Monica.
Mwanahabari Jacque Maribe, ambaye alishtakiwa pamoja na Irungu, hata hivyo aliondolewa mashtaka ya mauaji, huku hakimu akisema kuwa shtaka la mauaji sio shtaka sahihi ambalo upande wa mashtaka ungependekeza dhidi yake.
“Baada ya kuzingatia ushahidi uliotolewa upande wa mashtaka umetoa ushahidi wa kutosha na umedhihirisha kuwa mtuhumiwa alitekeleza mauaji,” Hakimu Grace Nzioka alisema katika uamuzi wake.
Katika kesi ya Maribe, hakimu aliamua kwamba ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka dhidi yake haukumweka katika nyumba ya marehemu usiku wa mauaji hatua iliyopelekea aondolewe mashtaka ya mauaji.
Jaji huyo hata hivyo alisema kwamba Maribe alikosea kutoa taarifa za uongo kwa maafisa wa upelelezi. Kuhusiana na kosa hili, hakimu alisema kuwa ni jukumu la afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma kuamua ni hatua gani ichukuliwe dhidi yake