Rais William Ruto atia saini Mswada tata wa Nyumba za bei nafuu

Mswada huo uliidhinishwa na Seneti na Bunge la Kitaifa wiki jana na marekebisho kadhaa ikiwa ni pamoja na kujumuisha serikali za kaunti.

Muhtasari

• Ushuru huo ulikuwa umetangazwa na Mahakama Kuu mwaka 2023 kuwa kinyume na katiba na kisha Mahakama ya Rufaa ikakubali uamuzi huo ikishikilia kuwa tozo hiyo ililetwa bila utaratibu wa kisheria.

Rais William Ruto aidhinisha Mswada wa Fedha wa 2023 Ikulu Juni 26, 2023.
Rais William Ruto aidhinisha Mswada wa Fedha wa 2023 Ikulu Juni 26, 2023.
Image: PCS

Rais William Ruto ametia saini Mswada tata wa Nyumba za bei nafuu.

Hafla hiyo ilifanyika katika Ikulu ya Nairobi mnamo Jumanne, ili kuandaa njia ya kurejeshwa kwa makato ya ada ya nyumba.

Mswada huo uliidhinishwa na Seneti na Bunge la Kitaifa wiki jana na marekebisho kadhaa ikiwa ni pamoja na kujumuisha serikali za kaunti.

Waajiri na waajiriwa wote watatoa makato ya 1.5% kutoka kwa mishahara yao ya kila mwezi.

Ushuru huo ulikuwa umetangazwa na Mahakama Kuu mwaka 2023 kuwa kinyume na katiba na kisha Mahakama ya Rufaa ikakubali uamuzi huo ikishikilia kuwa tozo hiyo ililetwa bila utaratibu wa kisheria.

Muswada huo unaweka vtinge vinne vya Nyumba za bei nafuu.

Vinajumuisha Kitengo cha Makazi ya Kijamii kwa watu wanaopata chini ya Ksh.20,000, kitengo cha kati kwa watu wanaopata zaidi ya Ksh.49,000, Makazi ya bei nafuu kwa wale wanaopata kati ya Ksh.20,000 hadi Ksh.149,000 na Makazi ya Vijijini kwa wale wanaoishi nje ya maeneo ya mijini.

Baadhi ya taasisi zitakazopewa jukumu la kutekeleza mradi wa Nyumba ni pamoja na Wizara ya Nyumba, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), serikali za Kaunti na Mashirika ya Kibinafsi kama ilivyoidhinishwa na bodi ya usimamizi wa hazina hiyo; Bodi ya Nyumba za bei nafuu.