Wanafunzi 11 wa Chuo Kikuu cha Kenyatta wafariki katika ajali mbaya ya barabarani Voi

Wanafunzi 42 walipata majeraha mabaya huku wanne wakiwa na majeraha madogo.

Muhtasari

•Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Voi Ibrahim Daffala, alisema wanafunzi 10 walifariki papo hapo huku mwingine akikata roho hospitalini.

•Basi la shule lilikuwa limebeba wanafunzi wa afya ya umma waliokuwa wakielekea Mombasa kwa safari ya kimasomo.

lililohusika katika ajali.
Basi lililohusika katika ajali.
Image: HISANI

Takriban wanafunzi 11 wa Chuo Kikuu cha Kenyatta walifariki Jumatatu jioni katika ajali mbaya ya barabarani iliyohusisha basi lao la shule na trela, Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Voi Ibrahim Daffala amethibitisha.

Daffala alisema wanafunzi 10 walifariki papo hapo huku mwingine akikata roho hospitalini.

Wanafunzi 42 walipata majeraha mabaya huku wanne wakiwa na majeraha madogo.

"Ajali hiyo ilitokea wakati mvua kubwa ilikuwa ikinyesha. Lori lilijaribu kuondoka kutoka barabarani ili kuepuka mgongano wa uso kwa uso na kusababisha ajali," Daffala alisema.

Picha zilizofikia Radio Jambo zinaonyesha basi la shule liligongwa upande wa kushoto.

Ajali hiyo inasemekana ilitokea eneo la Maungu, Voi, kaunti ya Taita Taveta, kando ya barabara kuu ya Mombasa-Nairobi.

Basi hilo la shule lilikuwa limebeba wanafunzi wa afya ya umma waliokuwa wakielekea Mombasa kwa safari ya kimasomo.

Trela ​​hilo lilikuwa likielekea Nairobi wakati ajali hiyo ilipotokea.

Basi la shule lilikuwa limebeba abiria 58.

Wanafunzi wapatao wanne walinusurika bila majeraha. Walipelekwa katika Kituo cha Polisi cha Maungu wakisubiri taratibu zaidi.

Makumi ya abiria wa basi hilo waliokuwa wamejeruhiwa walikimbizwa katika hospitali ya rufaa ya Moi, eneo la Voi.

Timu ya wataalam mbalimbali ilifika katika eneo la tukio kwa ajili ya kufanya uokoaji.

Daffala aliwashauri madereva wanaotumia barabara kuu ya Mombasa- Nairobi kuwa waangalifu kufuatia mvua kubwa inayonyesha kati ya Voi na Samburu.