Dj maarufu wa Kenya akamatwa kwa madai ya kumpiga afisa mkuu wa polisi hadi kufa

Maafisa watatu pia walikamatwa Jumamosi jioni kuhusiana na kisa hicho.

Muhtasari

•Washukiwa hao ambao wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Kabete wanadaiwa kumvamia na kumjeruhi inspekta Felix Kelian Kentos.

•Shambulio lilitokea baada ya afisa huyo kuhusika katika ajali ya barabarani isiyokuwa na majeraha mwendo wa saa kumi asubuhi katika soko la Kikuyu.

Marehemu Inspekta Felix Kelian Kentos.
Image: HISANI

Dj mashuhuri wa Kenya ni miongoni mwa washukiwa saba waliokamatwa kuhusiana na kifo cha afisa mkuu wa DCI.

Washukiwa hao ambao wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Kabete wanadaiwa kumvamia na kumjeruhi inspekta Felix Kelian Kentos.

Maafisa watatu walioko katika Kituo cha Polisi cha Kikuyu walikamatwa Jumamosi jioni kuhusiana na kisa hicho.

Watatu hao ni; Khadija Abdi Wako, Sammy Rotich Cherono, na Agnes Kerubo Mugo, na kwa sasa wanazuiliwa kama washukiwa wa mauaji ya askari mkuu.

Polisi walisema baadhi ya wahudumu wa DJ huyo ambao walimvamia Inspekta Felix Kelian Kentos mnamo Machi 16, 2024, pia wako kizuizini.

Polisi walisema DJ huyo alichukuliwa siku ya Ijumaa pamoja na mlinzi wake, dereva na mpiga picha wake baada ya kudaiwa kumvamia na kumshambulia vibaya Kelian wakiwa na hasira barabarani.

Waendesha bodaboda waliokuwepo wakati wa kisa hicho pia wanatafutwa, polisi walisema.

Shambulio hilo lilitokea baada ya afisa huyo kuhusika katika ajali ya barabarani isiyokuwa na majeraha mwendo wa saa kumi asubuhi katika soko la Kikuyu.

Kelian hakujitambulisha kama afisa wakati wa mzozo.

Polisi wa trafiki walihudhuria eneo hilo dakika chache baadaye.

Afisa huyo alifariki siku ya Ijumaa alipokuwa akipokea matibabu katika hospitali ya Nairobi West.

Alikuwa amelazwa na alikuwa akiendelea na matibabu ya maumivu ya tumbo na majeraha mengine aliyoyapata baada ya madai ya kupigwa.

Mwili wake ulihamishwa hadi kwenye Mochari ya Umash huku uchunguzi kuhusu suala hilo ukiendelea.

Habari za kifo cha afisa huyo ziliwashtua wenzake wengi baadhi yao waliotembelea msiba huo siku ya Jumamosi.

Mkuu wa polisi wa Nairobi Adamson Bungei alisema wanachunguza kisa hicho.