Chuo Kikuu cha Kenyatta kimejitokeza kuomba msaada wa kifedha kufuatia ajali mbaya iliyotokea katika eneo la Maungu, Voi mnamo Machi 18, 2024.
Wanafunzi 11 walipoteza maisha na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya basi la shule ya Chuo Kikuu cha Kenyatta kugongwa na trela kwenye barabara kuu ya Nairobi-Mombasa takriban wiki moja iliyopita. Basi hilo lilikuwa likiwapeleka wanafunzi na wafanyikazi kadhaa jijini Mombasa kwa ziara ya kimasomo.
Katika taarifa yake siku ya Jumamosi, taasisi hiyo ilieleza kuwa tukio hilo la kusikitisha limekuwa pigo kubwa na usaidizi wa kugharamia mazishi na matibabu kwa waathiriwa.
"Chuo kikuu cha Kenyatta kinawasiliana nawe kwa unyenyekevu ili kuomba usaidizi wa kifedha kufuatia ajali mbaya ya barabarani iliyotokea katika eneo la Maungu, Voi iliyogharimu wanafunzi 11 na kuwaacha majeruhi wengi," Taarifa iliyotolewa na KU Jumamosi ilisoma.
“Janga hilo limeacha jamii yetu ya KU ikitikiswa. Tunaomba usaidizi wako kwa wote walioathiriwa ili kusaidia kulipia gharama za matibabu, mazishi na nyinginezo. Tunashukuru kwa dhati maombi, mawazo na huruma zako kwa wakati huu.”
Michango itatumwa kupitia Benki ya Equity, jina la akaunti Chuo Kikuu cha Kenyatta, nambari ya akaunti 113029662073 au MPESA Paybill 247247, akaunti 113029662073.
Haya yanajiri takriban wiki moja baada ya kutokea kwa ajali mbaya ya barabarani iliyogharimu maisha ya wanafunzi 11 wa Chuo Kikuu cha Kenyatta na kuwaacha wengine kadhaa na majeraha.
Siku chache zilizopita, taasisi hiyo ilifichua kuwa ajali hiyo ilihusisha wanafunzi kutoka idara ya usimamizi wa afya na habari katika Shule ya Sayansi ya Afya.
Ilisema pamoja na wanafunzi kumi na mmoja waliopoteza maisha, wengine kumi na moja walijeruhiwa vibaya huku 16 wakipata majeraha madogo.
"Mipango inafanywa kusafirisha miili ya wanafunzi kumi na mmoja (11) hadi Mochari ya Chuo Kikuu cha Kenyatta kando ya Thika Super Highway," taasisi hiyo ilisema.