Easy Coach watoa taarifa baada ya basi yao kupata ajali iliyoua mwanafunzi mmoja

Kampuni hiyo imethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuahidi kutoa taarifa ya kina hapo baadae.

Muhtasari
  • Mwanafunzi mmoja kutoka Shule ya Upili ya Wavulana ya Chavakali amefariki na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya ajali hiyo ya basi.
Basi ya Easy Coach
Image: Hisani

Easy Coach wametoa taarifa baada ya ajali iliyohusisha basi lao kutokea katika  eneo la Maboleo, Kaunti ya Kisumu.

Kampuni hiyo ya mabasi imethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuahidi kutoa taarifa ya kina baadaye.

Basi hilo lilikuwa likisafiri kupitia njia ya Mbale-Nairobi.

Taarifa ya Easy Coach
Image: Hisani

Basi hilo lilikuwa limebeba wanafunzi kutoka shule ya upili ya Chavakali Boys waliokuwa wakienda nyumbani kwa Likizo ya Aprili.

Mwanafunzi mmoja kutoka Shule ya Upili ya Wavulana ya Chavakali amefariki na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya ajali hiyo ya basi.

Wanafunzi wawili walipata majeraha mabaya na kwa sasa wamelazwa katika Hospitali ya Avenue, Kisumu huku wengine 33 wakiendelea na matibabu katika Hospitali ya Mafundisho na Rufaa ya Jaramogi Oginga mjini Kisumu huku wengine kuruhusiwa kuenda nyumbani baada ya kupokea matibabu.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Kituo cha Polisi cha Kondele, dereva wa basi hilo hakupatikana eneo la tukio.

"Ilitokea kwamba gari lilikuwa likijadiliana na waasi wa Coptic wakielekea Kisumu kutoka Kakamega wakati dereva alishindwa kulimudu na kugonga  ulinzi wa reli na gari likaanguka kwenye ukingo wa barabara na kupumzika upande wake wa kushoto," taarifa za polisi kuhusu ajali hiyo.

Kulingana na shahidi Stephen Wasuna, basi hilo lilianguka kwa kishindo kikubwa, hali iliyowatia hofu wakazi wa karibu. Wenyeji waliwasaidia polisi kuwaokoa wanafunzi hao waliokuwa wamenaswa, na kisha kusafirishwa hadi hospitalini kwa kutumia magari ya polisi na ambulansi.

Mwili wa mwanafunzi huyo umehifadhiwa katika chumba cha maiti cha hospitali kwa taratibu zaidi. Aidha, mamlaka imeliondoa gari lililohusika katika ajali hiyo hadi kituo cha polisi cha Kondele kwa uchunguzi unaoendelea.