Mvulana wa miaka 6 afariki, dadake alazwa ICU baada ya kula mihogo yenye sumu Nyamira

Naomi Kerubo na watoto wake wanne walikula mihogo inayoshukiwa kuwa na sumu aliyopata kutoka kwa jirani.

Muhtasari

•Mtoto mwenye umri wa miaka sita alipoteza maisha huku wanafamilia wengine wakilazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Nyamira .

•Naomi na watoto wengine wawili walitibiwa na kuruhusiwa kuondoka Jumatatu.

Naomi Kerubo ambaye alimpoteza mwanawe baada ya familia yake kula mihogo inayoshukiwa kuwa na sumu.
Naomi Kerubo ambaye alimpoteza mwanawe baada ya familia yake kula mihogo inayoshukiwa kuwa na sumu.
Image: ALVIN RATEMO

Mtoto mwenye umri wa miaka sita alipoteza maisha huku wanafamilia wengine wakilazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Nyamira baada ya kula mihogo inayoshukiwa kuwa na sumu.

Naomi Kerubo na watoto wake wanne walikula mihogo inayoshukiwa kuwa na sumu ambayo aliipata kutoka kwa jirani ambapo alifanya kazi ya kibarua siku ya Jumapili.

"Nilikuwa nimeenda kufanya kazi katika shamba la karibu kama mtu wa kawaida wa kuajiriwa kwa siku hiyo. Baada ya hapo jirani akaniomba niletee mihogo kwa ajili ya chakula cha mchana,” alisema.

Mwendo wa saa kumi na mbili jioni, Naomi na watoto wake walianza kupata maumivu ya tumbo, kuhara, kutapika na kizunguzungu.

Mmoja wa watoto wake, ambaye sasa ameaga dunia alianguka, jambo lililomfanya Naomi kuomba usaidizi kutoka kwa majirani waliomkimbiza yeye na watoto wengine katika hospitali ya kaunti ndogo ya Ekerenyo kwa matibabu.

Huko Ekerenyo watano hao walipata huduma ya kwanza kabla ya kupelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Nyamira kwa matibabu maalum, ambapo mvulana huyo wa miaka sita alifariki.

Mtoto mwingine amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi lakini Naomi na watoto wengine wawili walitibiwa na kuruhusiwa kuondoka Jumatatu.

Kaimu afisa msimamizi wa Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Nyamira Angela Ogendi alisema mama huyo na watoto hao wawili wako katika hali nzuri.

"Yule aliye katika ICU anaimarika na atakapokuwa sawa tutampeleka katika wadi ya kawaida, wanafamilia wengine wako katika hali shwari," Ogendi alisema.

Nyumbani kwa Naomi mipango ya mazishi ya mtoto wake inafanyika, na majirani wametoa wito kwa wataalam kusaidia kujua kama muhogo ambao familia ilikula ulikuwa unafaa kwa matumizi.

“Tumepanda mihogo na tumekuwa tukitumia mihogo, lakini hatujawahi kupata kifo kwa kuchukua mihogo. Hili ni tukio la kwanza la aina hii kutokea katika eneo letu na sote tumeshtuka," Rister Ongwanka mkazi alisema.

"Tunaomba wataalam watusaidie kujua jinsi mihogo ambayo familia hii ilikula iliishia kusababisha vifo na madhara ya kiafya."