Watu kadhaa wahofiwa kufariki, wengine wengi kujeruhiwa baada ya basi kubingirika katika daraja la Nithi

Kwingineko, watu 5 waliuawa kufuatia ajali ya magari mengi iliyohusisha lori kadhaa eneo la Timboroa.

Muhtasari

•Ajali hiyo ilihusisha basi lililokuwa likitoka Meru kuelekea Nairobi katika daraja la Tharaka Nithi siku ya Jumapili adhuhuri.

•Shahidi alidai kuwa ameona watu wasiopungua watatu waliofariki. Kuna hofu kwamba idadi inaweza kuongezeka.

Eneo la ajali ya daraja la Nithi Jumapili adhuhuri
Image: HISANI

Kamanda wa polisi kaunti ya Tharaka Nithi Zachaeus Ngeno amethibitisha kutokea kwa ajali ambapo abiria kadhaa wanahofiwa kufariki na wengine wengi kujeruhiwa.

Ajali hiyo ilihusisha basi lililokuwa likitoka Meru kuelekea Nairobi katika daraja la Tharaka Nithi siku ya Jumapili adhuhuri.

Ngeno alisema sababu ya ajali hiyo bado haijajulikana huku maafisa wa polisi wakianza uchunguzi wa ajali hiyo mbaya.

"Bado tunafanya uchunguzi kubaini idadi ya walioaga dunia lakini tuna uhakika kwamba kulikuwa na vifo," Ngeno alisema.

Baadhi ya abiria walioumia walipelekwa katika hospitali za karibu kwa matibabu.

Mkuu huyo wa polisi wa kaunti aliwataka madereva kuwa waangalifu zaidi na kuhakikisha magari yao yako katika hali nzuri ili kuepusha ajali.

Hata hivyo, shahidi alidai kuwa ameona watu wasiopungua watatu waliofariki. Kuna hofu kwamba idadi inaweza kuongezeka.

Hadi kufikia kuchapishwa kwa habari hii, shughuli za uokoaji zilikuwa bado zinaendelea huku madaktari wakionekana kwenye eneo la tukio.

Kwingineko, watu watano waliuawa kufuatia ajali ya magari mengi iliyohusisha lori kadhaa eneo la Timboroa, Baringo kwenye Barabara kuu ya Nakuru-Eldoret.

Ajali hiyo ilisababisha msongamano mkubwa wa magari katika barabara kuu yenye shughuli nyingi huku mvua zikitatiza shughuli za uokoaji.

Ajali hizo ni za hivi punde ambazo zimegharimu maisha ya watu wengi lakini kuna kampeni ya kukabiliana na hali hiyo.