Chama cha Orange Democratic Movement kimedai kuimarishwa ulinzi wa Gavana wa Kisii Simba Arati kufuatia madai ya kunyanyaswa na polisi.
Katika taarifa ya Jumatatu, ODM pia ilitaka hatua za haraka zichukuliwe dhidi ya wanaohusika na unyanyasaji huo.
"Tunamtaka Arati apewe ulinzi wa hali ya juu inavyotakiwa na sheria na hatua zichukuliwe dhidi ya wahusika wa mipango hiyo haramu na vitisho kwa maisha yake," chama hicho kilisema.
Chama hicho kilieleza masikitiko yake kwamba serikali bado haijachukua hatua tangu kuibuka kwa klipu ya sauti iliyovuja ya mazungumzo ya simu kati ya Arati, makamu mwenyekiti wa chama hicho na mtu anayedaiwa kuwa afisa mkuu wa polisi.
Katika klipu hiyo ya dakika tano, mtu huyo anasikika akizungumzia mpango wa polisi "kusimamia" hali ya kisiasa katika Kaunti ya Kisii.
Sauti katika klipu hiyo inasikika ikitoa amri kwa Arati na wafuasi wake kushughulikiwa.
Kama sehemu ya uchunguzi wa madai ya vitisho, serikali kupitia Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) iliomba hati za upekuzi katika nyumba au nyumba za wafuasi 14 wa Arati.
Katika maombi mseto mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkuu mjini Kisii, DCI alidai kuwa watu hao 14 wanamiliki silaha haramu ambazo zilitumiwa kutekeleza uhalifu katika kaunti hiyo.