Mshangao huku mwanawe Ogolla akiwafariji waombolezaji, afichua kwa nini familia haina huzuni

Joel ambaye alionekana kuwa ametulia aliwataka waombolezaji waache kuwa na huzuni kufuatia kifo cha baba yake.

Muhtasari

•Joel Ogolla aliwashangaza waombolezaji waliofika nyumbani kwao siku ya Ijumaa jioni kwa kuchukua muda kuwafariji.

•Kijana huyo alibainisha kuwa baba yake yuko mahali pazuri hata katika kifo chake.

watazama rais William Ruto akijaza kitabu cha waombolezaji mnamo Aprili 19, 2024.
Mjane wa Francis Ogolla, Rachel Ruto na Joel Rabuku Ogolla watazama rais William Ruto akijaza kitabu cha waombolezaji mnamo Aprili 19, 2024.
Image: PCS

Bw Joel Rabuku Ogolla, mtoto wa marehemu Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Francis Ogolla, aliwashangaza waombolezaji waliofika nyumbani kwao siku ya Ijumaa jioni kwa kuchukua muda kuwafariji.

Baadhi ya watu mashuhuri akiwemo Rais William Ruto walizuru nyumbani kwa marehemu Ogolla jijini Nairobi siku ya Ijumaa ili kuwapa rambirambi familia katika nyakati hizi ngumu.

Alipopewa nafasi ya kuwahutubia waombolezaji, Joel ambaye alionekana kuwa ametulia kwa mshangao alianza kuwafariji na kuwataka waache kuwa na huzuni kufuatia kifo cha baba yake. Alisema marehemu aliwaandaa vyema kuhusu kifo chake na akabainisha kuwa endapo baba yake angeamka angejiuliza kwa nini watu wana huzuni.

"Yangu ni kusema hivi karibuni kila mtu. Ninaona nyuso nyingi za huzuni lakini jenerali angekuwa anashangaa watu wana huzuni kwa nini, hasa kwa vile ametutayarisha kwa siku hii kwa muda mrefu sana,” Joel aliwaambia waombolezaji.

Aliendelea, “Nyinyi watu, tafadhali muwe na furaha zaidi. Sisi kama familia tunaegemea imani yake, imani yetu wenyewe na imani ya Yesu Kristo ambaye alikuwa mwamba wake wa pembeni, nguzo yake na kila kitu.”

Kijana huyo alibainisha kuwa baba yake yuko mahali pazuri hata katika kifo chake. Alisema aliuona mwili wa mzazi huyo wake na akabaini kuwa alifariki akiwa na tabasamu la kicheshi ambalo alikuwa nalo kila mara.

“Kwa hiyo nyinyi msivurute sura sana, ilhali yeye hadi katika kifo anashangaa shida ni nini na hawa watu.. Itakuwa sawa kwa sisi sote, "Joel alisema.

"Poleni sana, kila mtu hapa alikuwa na uhusiano naye, jisikie unakaribishwa na karibuni sana," aliongeza.

Marehemu Mkuu wa Majeshi (CDF) Francis Ogolla, 62, anatazamiwa kuzikwa nyumbani kwake Ng’iya huko Alego Usonga mnamo Aprili 21.

Hii ni kwa mujibu wa familia yake.

Familia pia ilifichua kwamba mazishi hayo yanakuja mapema kwa sababu Jenerali Ogolla alikuwa ameacha wosia na maagizo kwamba azikwe ndani ya saa 72 baada ya kifo chake.

Duru zilisema kuwa wanajeshi wamearifiwa kuhusu wosia huo na kufanya kazi ndani ya muda uliopangwa ili kuhakikisha kuwa unaheshimiwa.

Maandalizi ya mazishi yamechukuliwa na serikali. Hii ni kwa sababu alifariki akiwa ofisini.