Maseneta wakosoa jinsi Sonko alivyong'atuliwa mamlakani

Maseneta walisema kuna haja ya kuhakikisha magavana hawaondolewi afisini kwa njia isiyo ya haki.

Muhtasari

•Baadhi ya maseneta waliibua wasiwasi kuhusu jinsi aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko aliondolewa afisini.

•Muswada unalenga kuwalinda Magavana na watendaji wa Kaunti dhidi ya kuondolewa madarakani ambako sio kwa lazima.

Bunge la Seneti
Image: EZEKIEL AMING'A

Bunge la Seneti limeanza mjadala kuhusu Muswada unaolenga kuongeza viwango vinavyohitajika kuafikiwa na mabunge ya kaunti ili  kumtimua gavana, na mawaziri wake.

Wakati wa mjadala kuhusu Mswada wa Marekebisho ya Serikali za Kaunti unaolenga kuongeza kizingiti cha kutimuliwa kwa Magavana katika Bunge la Kaunti, baadhi ya maseneta waliibua wasiwasi kuhusu jinsi aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko aliondolewa afisini.

Maseneta hao walisema kuna haja ya kuhakikisha magavana hawaondolewi afisini kwa njia  isiyo ya haki.

Seneta wa Kericho Aaron Cheruiyot alisema kuna haja ya kuwa na sheria ambayo itahakikisha viongozi wa kaunti wanatendewa haki.

"Ilidhihirika hapa kuwa kizingiti cha kuondolewa kwa aliyekuwa Gavana Sonko hakikuafikiwa katika Bunge la Kaunti ya Nairobi ilhali kuna mambo mengi yanayotokea katika zoezi la kuondoa gavana mamlakani," Seneta Cheruiyot alisema.

"Kutimuliana mamlakani kumekuwa mchakato wa kisiasa lakini una madhara makubwa na ya kisheria."

Wakati wa kikao hicho, maseneta walikuwa wakijadili Mswada wa Serikali za Kaunti (Marekebisho) unaolenga kuongeza kizingiti cha kuondolewa kwa gavana kutoka thuluthi hadi thuluthi mbili.

"Ninapenda ukweli kwamba tunaongeza kizingiti. Kufikia wakati thuluthi mbili ya bunge inakubali kuwa kuna kitu kibaya kwako, basi kuna tatizo mahali fulani. Theluthi moja ilikuwa chini sana," Seneta Cheruiyot aliongeza.

Mswada wa Marekebisho ya Serikali za Kaunti unafadhiliwa na Seneta wa Nandi Samson Cherargei.

Unalenga kuwalinda Magavana na watendaji wa Kaunti dhidi ya kuondolewa madarakani ambako sio kwa lazima.

Katika mada yake, Seneta wa Kitui Enoch Wambua pia aliunga mkono Mswada huo akisema umecheleweshwa kwa muda mrefu.

“Tumeona magavana wakipitia machungu na uchungu wa kuondolewa mamlakani kwa sababu tofauti na kipengee cha katiba kuhusu kuondolewa kwa magavana,” alisema.

"Kufikia sasa, ninaamini hakukuwa na sababu za kumwondoa Gavana Sonko afisini. Ninaamini aliondolewa afisini kwa sababu nyingine na wala si uvunjaji wa katiba."

Alisikitika kwamba uamuzi huo ulimpotezea gavana huyo wa zamani kiasi kwamba hangeweza kushikilia wadhifa wa umma.

Seneta Wambua aliitaka kamati ya ugatuzi kuchukulia suala hilo kwa uzito ili kuokoa viongozi kutoka kwa dhiki na machungu zaidi.

"Mheshimiwa Spika, kiongozi kijana sana, shupavu na mtu wa watu hawezi kushika wadhifa huo kwa sababu aliondolewa madarakani kwa sababu za ziada."

"Acheni kamati ya ugatuzi ishughulikie suala hili na kuleta mswada mwafaka kuhusu kuondolewa mamlakani kwa gavana."

Wambua alisema kuna haja ya kuwa na sheria ya kuondoana mamlakani kwa mashtaka dhabiti ili kuwazuia wanasiasa kutumia hatua ya kung'atuana mamlakani ili kutatua masuala ya kisiasa.

Seneta wa Machakos Agnes Kavindu Muthama aliunga mkono mswada huo akisema wengi wameangukia kwenye shida hiyo.

Alisema sheria iliyokusudiwa inapaswa kulindwa dhidi ya maelewano na Seneti au mabunge ya kaunti.

Wengine waliounga mkono Mswada huo ni pamoja na; Seneta wa Makueni Dan Maanzo, Seneta wa Kiambu Karungo Wa Thangwa, Seneta wa Marsabit Mohammed Chute na Seneta mteule Beth Syengo.

Kwa upande wake, Maanzo alisema Mswada huo unapaswa kupitishwa bila marekebisho.

"Mswada umeandaliwa vyema na ni mzuri kwa taifa, ili tuweze kulinda haki za watu wengine na hasa haki za ajira na kuwalinda dhidi ya uwindaji wa wachawi wa kisiasa," Maanzo alisema.

Thangwa pia aliongeza kuwa ikiwa Mswada huo ungekuwepo, Magavana waliotimuliwa kama Sonko wangepewa fursa ya kumaliza rufaa zao.

Seneta Syengo kwa upande wake aliongeza kuwa Sonko aliondolewa afisini chini ya misingi isiyoeleweka.

“Kuondolewa mamlakani kwa Sonko kulitokana na maslahi ya kisiasa au chuki ya kibinafsi. Ni muhimu kuwa na sababu zilizo wazi na tunapaswa kuongeza kizingiti hiki cha kufunguliwa mashtaka, "alisema.