Sabreen alikuwa amekufa kabla kumtazama machoni mwanawe au kumbeba.
Mama huyo mwenye umri mdogo alikuwa amebeba mtoto wake kwa miezi saba na nusu ya ujauzito.
Zilikuwa siku zenye hofu ya kila mara, lakini Sabreen alitumaini kwamba bahati ya familia hiyo ingedumu hadi vita viishe.
Bahati hiyo ilitoweka kutokana na kishindo na moto wa mlipuko saa moja kabla ya saa sita usiku tarehe 20 Aprili.
Waisraeli walirusha bomu kwenye nyumba ya familia ya al-Sakani huko Rafah ambapo Sabreen, pamoja na mumewe na binti mwingine wa wanandoa hao - Malak wa miaka mitatu - walikuwa wamelala.
Sabreen alipata majeraha makubwa na mumewe na Malak waliuawa, lakini mtoto alikuwa bado hai tumboni mwa mamake wakati waokoaji walipofika eneo hilo.
Walimkimbiza Sabreen hospitalini, ambapo madaktari walimfanyia upasuaji wa dharura ili kujifungua mtoto.
Sabreen hakuweza kuokolewa lakini madaktari walifanya kazi ya kumfufua mtoto, wakigonga kifua chake taratibu ili kuamsha kupumua.
Hewa ilisukumwa kwenye mapafu yake."Alizaliwa katika hali mbaya ya kupumua," Dkt Mohammed Salama, mkuu wa kitengo cha dharura cha watoto wachanga katika Hospitali ya Emirati huko Rafah.
Lakini mtoto huyo - ambaye alikuwa na uzani wa kilo 1.4 tu (pauni 3.1) - alinusurika na mateso ya kuzaliwa kwake.Daktari aliandika "mtoto wa shahidi Sabreen al-Sakani" kwenye kipande cha kanda na kukiambatanisha na mwili wake.
Kisha akawekwa kwenye incubator."Tunaweza kusema kuna maendeleo fulani katika hali yake ya afya," Dk Salama alisema.