MCA wa Mara ahofia maisha yake baada ya kushambuliwa Narok

Seneta Cherargei alikashifu kushambuliwa kwa Kipng’eno na kumtaka gavana Ole Ntutu kuruhusu uhuru wa kujieleza katika kaunti hiyo.

Muhtasari

• MCA huyo amekuwa akimpigia debe mbunge wa Narok Magharibi Gabriel Tongoyo kutwaa uongozi wa UDA katika kaunti ya Narok.

Mwakilishi wa wadi ya Mara katika kaunti ya Narok Chepkwony Kipng’eno, akizungumza baada ya kuandikisha taarifa kwa polisi/ 24/04.2024.
Mwakilishi wa wadi ya Mara katika kaunti ya Narok Chepkwony Kipng’eno, akizungumza baada ya kuandikisha taarifa kwa polisi/ 24/04.2024.
Image: SCREENGRAB

Mwakilishi wa wadi ya Mara katika kaunti ya Narok Chepkwony Kipng’eno anadai kuwa maisha yake yamo hatarini.

Kipng’eno siku ya Jumatano aliandikisha taarifa kwa polisi baada ya kushambuliwa na watu aliodai ni mahasimu wake wa siasa na kupokea vitisho kwa maisha yake.

Kipng’eno aliripotiwa kushambuliwa wakati akihudhuria hafla ya mazishi kwa kile alidai ni ukosoaji wake dhidi ya gavana Patrick Ntutu wa Narok pamoja na msimamo wake kuhusiana na uchaguzi wa mashinani wa chama cha UDA.

MCA huyo amekuwa akimpigia debe mbunge wa Narok Magharibi Gabriel Tongoyo kutwaa uongozi wa UDA katika kaunti ya Narok.

Inadaiwa Kipng’eno alikabiliwa na kundi moja la vijana kwa kuhoji hazina ya wadi ya shilingi milioni 100 iliyotangazwa na serikali ya kaunti akisema hakukuwa na miradi katika wadi zote inayoashiria matumizi ya mamilioni ya pesa zinazosemekana kuwekezwa huko.

“Na ningependa kuzungumzia kauli ya mzungumzaji mmoja wa hapa aliyesema Shilingi milioni 100 zimetumika kwenye wadi hizo, lakini kwa nini hakuna barabara katika maeneo haya ikiwa kweli fedha hizi zilifika kwenye wadi,” MCA huyo alisema.

Tukio hili pia lilipenyeza hadi katika ukumbi wa seneti huku Seneta wa Nandi Samson Cherargei na mwenzake wa Narok Ledama Ole Kina wakimkosoa gavana Ntutu kwa kumdhalilisha mwakilishi wadi wa Mara kwa kuwa na maoni kinzani na yake.

Gavana wa Narok Patrick ole Ntutu.
Gavana wa Narok Patrick ole Ntutu.
Image: KIPLANGAT KIRUI

Cherargei alikashifu tukio la kushambuliwa kwa Kipng’eno na kutoa wito kwa gavana Patrick Ole Ntutu kuruhusu uhuru wa kujieleza katika kaunti hiyo.

“Mheshimiwa alikuwa anapigwa anazabwa makofi, na si mara ya kwanza, nilikuwa naona yule gavana alitoka Tunai alikuwa na heshima na maswali, sijui gavana wa sasa Ntutu ameanza kuwa mtukutu ambaye huwezi kuuliza swali”, Cherargei alisema.

Akizungumza baada ya kurekodi taarifa kwa polisi katika afisi za Narok CID, MCA Kipng’eno alisema anahofia maisha yake baada ya kushambuliwa na jumbe za vitisho alizotumiwa kupitia simu yake ya rununu.

"Sasa ninahofia maisha yangu kufuatia vitisho..., na ndiyo maana niko hapa," mwakilishi wa wadi hiyo alisema alipohutubia wanahabari katika kituo cha polisi.

Kwa upande wake gavana Ntutu aliwaomba wafuasi wake kuachana na Kipng’eno akishikilia kwamba hana ubaya naye na kutoa wito kwa wananchi na vyongozi wote kufanya kazi kwa pamoja.

“Hata mkiona MCA wangu mmoja akienda kando tumuombee Mungu kwa sababu hii ni shida sisi tumeona kutoka zamani, ndio maana tumesema hata sisi wavijana wangu waache yeye tu aende...Chepkwony mimi sina ubaya na wewe,” Ntutu alisema.